Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa IDAI wasogezwa karibu na nyumbani - UNHCR

Familia ambazo ni manusura wa kimbunga Idai , zikihamishiwa kutoka makazi ya muda huko IFAPA mjini BEIRA kwenda kituo jirani na makazi yao ya awali wilayani Buzi nchini Msumbiji.
© UNHCR/Luiz Fernando Godinho
Familia ambazo ni manusura wa kimbunga Idai , zikihamishiwa kutoka makazi ya muda huko IFAPA mjini BEIRA kwenda kituo jirani na makazi yao ya awali wilayani Buzi nchini Msumbiji.

Manusura wa IDAI wasogezwa karibu na nyumbani - UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Familia zilizonusurika na kutawanywa na kimbunga Idai nchini Msumbiji zimeanza kuhamishiwa katika maeneo yaliyo karibu na mahali walikotoka wakati wa zahma hiyo. Kwa mujibu swa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR zoezi hilo linaendeshwa kwa ushirikiano na serikali ya Msumbiji na washirika wengine .

 Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema zoezi hilo lilianza mwishoni mwa wiki na hadi sasa“familia 200 zimeshashamishwa kutoka malazi ya dharura yaliyoko katikati mwa mji wa Beira. Na tunatumai kwamba katika siku 10 zijazo watu takriban 70,000 watahamishwa kutoka malazi ya dharura ambako wamekuwa wanaishi kwa mwezi mmoja uliopita maeneo hayo ni pamoja na shule, majumba ya burudani, maktaba na majengo mengine.”

UNHCR inasema watu hao wanahamishiwa kwenye maeneo kama Guara Guara ambayo ni ya mwinuko na ni bora zaidi kwa familia huizo kuanza maisha karibu na nyumbani walilokuwa wakiishi kabla ya kimbunga hadi pale watakapoweza kujimudu tena.

Kwa mujibu wa shirika hilo baada ya kuwasili makazi mapya familia hizo zinapatiwa mahema na makazi hayo yana huduma ya maji na vyoo na serikali kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP wanawagawia chakula.

Familia zinazowasili Guara Guara zitakuwepo hapo kwa siku tatu kisha zitapatiwa neo na vifaa vya kusafisha eneo hilo, vifaa vya ujenzi wa nyumba mpya na mbegu za kuanza kilimo.

UNHCR pia imekusanya akiba ya vifaa muhimu kama mablanketi, vyandarua vya mmbu, vyombo vya kupikia na madumu ya maji kwa ajili ya familia hizo , huku kipaumbele kikitolewa kwa watu wenye ulemavu, wanawake na Watoto wasio na wazazi au walezi.