Ni wakati wa kuijali dunia hii kwani sasa iko hatarini- Maria Fernanda Espinosa.

22 Aprili 2019

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa kupitia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya sayari Dunia yaliyofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani hii leo,  ametoa tahadhari kuwa “dunia yetu iko katika hatari kubwa na sasa ni wakati wa kuijali sayari hii.”

Akizungumzia sayari dunia, Bi Espinosa amesisitiza kuwa wanadamu wameihatarisha dunia na ni wakati wa kuukarabati uharibifu ambao umeshatokea ili kulinda na kurejesha mzunguko wake muhimu kuhakikisha tunayalinda maisha na asili iweze kujizaailisha tena na tena.

Kisha akarejelea kusema, “dunia endelevu ambayo ni sisi ni sehemu ya kufanikisha Agenda 2030 inatuhitaji kufikiria tena namna ambavyo tunachangamana na asili. Kutafuta uwiano kati ya mahitaji ya binadamu na rasilimali ambazo Dunia inatupatia, haina maana tusizitumie lakini inamaanisha kuwa tunatakiwa kusitisha matumizi mabaya ya rasilimali hizo, tujenge utaratibu ambao tunaheshimu vizingiti vilivyowekwa na asili, uwezo wake wa kujizalisha na pia haki yake ya kuwepo na kujidumisha yenyewe.”

Naye Naibu Waziri wa mazingira wa Bolivia Bi Cynthia Silva Maturana akizungumza katika mkutano huo amesema, “ni wakati wa kuzisihi asasi za kiraia, mashirika, watu, kujiruhusu kujenga mstakabali wa pamoja, kuchangia masuluhisho ya pamoja kwa ajili ya kutafuta majibu ya maswali mengi.”

Kwa upande wake Balozi wa India katika Umoja wa Mataifa Syed Akbaruddin amesema, “elimu ni jambo muhimu na la nguvu katika masuala ya kudhibiti hali ya hewa. Ni bahati nzuri kuwa kizazi kijacho kimeelimika vema na wana nia kukupunguza uchafuzi wa hewa kuliko kizazi chetu kilivyokuwa.”

Mnamo mwaka 2009, Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha kuwa kila tarehe 22 Aprili iwe siku ya kimataifa ya sayari mama dunia. Kwa kufanya hivyo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanatambua kuwa dunia na mazingira yake ndivyo makazi yetu na wakajiwekea nia ya kukuza kuchangamana na asili ili kuufikia usawa kati ya mahitaji ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa kizazi cha sasa na vijacho.

Katika majadiliano ya Baraza Kuu kuhusu maelewano ya wanadamu na asili, washiriki wameanza kwa dakika moja ya ukimya ili kuwakumbuka waliouawa katika mashambulizi la kigaidi yaliyotekelezwa jumapili ya Pasaka nchini Sri Lanka.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter