Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya walinda amani wa UN hayatazuia nia yetu kuisaidia Mali kupata amani-Antonio Guterres.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa kazini nchini Mali.
Harandane Dicko
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa kazini nchini Mali.

Mashambulizi dhidi ya walinda amani wa UN hayatazuia nia yetu kuisaidia Mali kupata amani-Antonio Guterres.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York Marekani amelaani shambulio dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa lililotekelezwa mapema leo nchini Mali, kuua mlinda amani mmoja na kujeruhi wengine wanne.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, leo jumamosi katikati mwa eneo la Mopti, shambulizi limefanywa dhidi ya walinda amani walipokuwa katika doria. Mlinda amani aliyefariki anatoka Misri. Wakati wa kukabiliana na tukio hilo, walinda amani wamemuua mshambuliaji mmoja na kufanikiwa kuwatia mbaroni wenzake nane.

Bwana Guterres amesema kuwa matukio ya namna hiyo hayatadhohofisha nia ya Umoja wa Mataifa kusaidia mamlaka za Mali katika kuifikia amani.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anakumbushia kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, yanaweza kuwa uhalifu wa kivita. Na matukio haya hayatadhohofisha nia ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kuwasaidia watu wa Mali na serikali yao kufikia amani na utulivu.”

Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu wa mlinda amani aliyepoteza maisha na pia kwa serikali ya Misri huku akiwatakia majeruhi kupona haraka.

Tweet URL

 

Naye Jean-Pierre Lacroix kupitia ukurasa wake wa Twitter ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo na akatuma salamu za rambirambi kwa familia ya askari aliyeuawa na akasisitiza kuwa askari huyo pamoja na wenzake walikuwa “wanatekeleza jukumu muhimu la kuulinda msafara.”

MINUSMA ilianzishwa mwaka 2013 ingawa eneo hilo limesalia kuwa la hatari dhidi ya operesheni za Umoja wa Mataifa. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2019, walinda amani wapatao 195 tayari wamepoteza maisha katika maeneo hayo.