Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu kwa watoto Msumbiji mashakani, kisa? Kimbunga Idai!

Wanawake kama hawa wenye uhitaji wanaangaziwa na huduma za hifadhi za jamii nchini Tanzania.
OCHA/Rita Maingi
Wanawake kama hawa wenye uhitaji wanaangaziwa na huduma za hifadhi za jamii nchini Tanzania.

Elimu kwa watoto Msumbiji mashakani, kisa? Kimbunga Idai!

Msaada wa Kibinadamu

Kimbunga Idai kilichopiga Msumbiji mwezi uliopita wa Machi kimesababisha zaidi ya watoto 305,000 nchini humo washindwe kuhudhuria shuleni.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF iliyotolewa leo mjini New York, Marekani na Beira Msumbiji imesema kama hiyo haitoshi vyumba 3,400 vya madarasa vimeharibiwa kabisa kwenye maeneo yaliyokumbwa na kimbunga hicho ikiwemo 2,713 jimboni Sofala pekee.

UNICEF inasema katika baadhi ya maeneo, shule zinahitaji ukarabati mkubwa kwasababu zilitumika kama makazi ya dharura kwa watoto na familia zao ambazo zilipoteza makazi.

Huku ikitaka ujenzi na ukarabati uwe imara ili kuhimili majanga ya asili siku za usoni, UNICEF inasihi wadau wa kibinadam ukuendelea kushirikiana kusaka suluhu ikiwemo kupata vituo vya muda vya watoto kujifunza ili angalau watoto waendelee na masomo haraka iwezekanavyo.

“Kuendelea kwa watoto kutokuwepo shuleni kwa muda mrefu, kunaweza kuwa na madhara makubwa ya muda mfupi na muda mrefu kwa watoto,” imesema taarifa hiyo.

Mtoto wa umri wa miaka 6 akiwa ameshika kabrasha lake la elimu alilolipokea kutoka UNICEF ikiwa ni sehemu ya msaada wa watoto na familia zilizoathiriwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji.
UNICEF/James Oatway
Mtoto wa umri wa miaka 6 akiwa ameshika kabrasha lake la elimu alilolipokea kutoka UNICEF ikiwa ni sehemu ya msaada wa watoto na familia zilizoathiriwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji.

UNICEF ina wasiwasi kuwa uharibifu wa miundombinu ya shule nchini Msumbiji  unaweza kuwa na madhara makubwa kwenye viwango vya uandikishaji watoto shuleni na kujifunza wakati  huu ambapo tayari viwango hivyo ni vya chini.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Msumbiji, idadi idadi ya watoto walioandikishwa kwa ajili ya shule ya sekondari ni chini ya asilimia 20.

Walimu nao, kwa mujibu wa UNICEF, wameathirika kutokana na kimbunga hicho kwa hiyo UNICEF inataka usaidizi pia uwalenge ikiwemo msaada wa fedha ili waweze kujenga upya maisha yao na hatimaye warejee kufundisha.

Tayari UNICEF inashirikiana na wadau kusaidia Watoto kurejea shuleni kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapatia vifaa vya shule na kujenga vituo vya muda vya kujifunzia, mahema na kukarabati mifumo ya maji safi na huduma za kujisafi.

UNICEF ili kufanikisha mipango hiyo Msumbiji na mataifa mengi ya Zimbabwe na Malawi yaliyokumbwa na kimbunga Idai, imeomba dola milioni 122 kwa ajili ya operesheni za miezi 9 ijayo.

Machi 24 mwaka 2019 nchini Msumbiji, mvulana akiwa amesimama karibu na nyumba iliyoharibiwa kufuatia mafuriko yaliyotokana na kimbunga idai mji wa Beira.
UNICEF/Prinsloo
Machi 24 mwaka 2019 nchini Msumbiji, mvulana akiwa amesimama karibu na nyumba iliyoharibiwa kufuatia mafuriko yaliyotokana na kimbunga idai mji wa Beira.