Watoto 6000 waunganishwa na familia zao nchini Sudan Kusini.

18 Aprili 2019

Idadi ya watoto waliouganishwa na familia zao nchini Sudan Kusini baada ya kutenganishwa kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwezi Disemba mwaka 2013 sasa imefikia 6000.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la Save the Children pamoja na wadau wao wamefanikiwa kufikia idadi hiyo baada ya mtoto Nyandor mwenye umri wa miaka 17 pamoja na nduguze  wanne wakiwemo dada wawili na kaka wawili kuunganishwa na familia zoa jana huko Bentiu kupitia mradi wa kuunganisha watoto na familia, au FTR.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa Juba, Sudan Kusini imesema ndugu hao watano walitenganishwa kutoka kwa wazazi wao wakati mashambulizi katika eneo la Bor mwaka 2014.

“Katikati ya mgogoro wanafamilia walikimbilia katika maeneo tofautitofauti na hawakuwa wameonana kqwa kipindi chote hicho lakini baada ya juhudi za wafanyakazi wa Save the Children, hatimaye jana wamekutana tena,” imesema taarifa hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Save the Children Sudan Kusini, Arshad Malik, anasema “ulikuwa wakati wa hisia kwa kila mtu aliyehusika, ilikuwa ni machozi, nyimbo na furaha. Kuona furaha katika nyuso zao baada ya kuyapitia mengi, inatujaza matumaini. Hatutaacha mpaka pale ambapo watoto wote waliotengana na familia zao watakapounganishwa tena.”

Taarifa ya UNICEF  imeeleza kuwa takribani miaka mitano ya mgogoro kumeshuhudiwa zaidi ya watu milioni nne wakiyahama makazi yao na watoto kuwapoteza wazazi wao.

Watoto wapatao 8,000 nchini humo bado haifahamiki waliko au bado wametengana na familia zao. Watoto waliotengana na familia zao wanakuwa hatarini zaidi na hiyo ndiyo maana inakuwa muhimu sana UNICEF na Save the Chirldren kuwatafuta na kuwakutanisha.

Mkataba wa amani uliofikiwa mwezi septemba mwaka 2018 umesababisha  wakimbizi waanze kurejea Sudan Kusini wakitokea nchi jirani.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud