Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka hatua kulinda watoto mitandaoni

UNICEF inachagiza matumizi bora ya intaneti na barubaru huko Dili, Timor-Leste
© UNICEF/UN067579/Gomes
UNICEF inachagiza matumizi bora ya intaneti na barubaru huko Dili, Timor-Leste

UN yataka hatua kulinda watoto mitandaoni

Haki za binadamu

Mtalaamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya faragha, Joe Cannataci hii leo mjini Geneva Uswisi, ameomba jitihada za pamoja za kimataifa za kulinda na kuwawezesha watoto kukabiliana na mazingira ya mtandaoni.

 Tayari Cannataci ameanzisha mpango wa miaka miwili, ikiwa ni pamoja na mashauriano ya mtandaoni na ya umma, kukusanya mapendekezo yenye lengo la kuboresha ulinzi kwa ajili ya faragha ya mtandaoni kwa watoto kote duniani kwa kuweka msisitizo juu ya ulinzi na tabia sahihi mitandaoni. 

Mapendekezo yatawasilishwa katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwaka 2021.

Aidha Bwana Cannataci amekaribisha maendeleo yaliyofikiwa Uingereza yakiwemo maelekezo ya serikali kuhusu mchakato wa kuanzisha kanuni mpya za ‘umri unaofaa’.

Amesema kuwa, “nimeweka kanuni mpya ya umri unaofaa kama moja ya ajenda za mkutano ujao wa mwezi Septemba kuhusu kampuni kutumia taarifa binafsi. Ninataka kusikia kutoka kwa vinywa vyao wenyewe kampuni kama Google, Apple, Facebook, Microsoft, Amazon, Twitter na kadhalika ikiwa mapendekezo yanayotengenezwa yanaweza na yanatakiwa kuwekwa katika uhalisia kote duniani na ikiwa ni hivyo, iwe kwa namna gani na lini.”

Mtaalamu maalum huyo wa Umoja wa Mataifa amewahimiza wadau wote kuchangia katika mashauriano yanayoendelea nchini Uingereza, akisema kuwa ushiriki wao unaweza kushawishi namna ambayo ulinzi kwa faragha za watoto mtandaoni zitakavyoanzishwa duniani kote.