Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli ya mkimbizi Kakuma kwamba bora elimu kuliko elimu bora ni ishara ya kiwango cha huduma hiyo-Onano

Vivian Onano, mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR.
UN News Kiswahili
Vivian Onano, mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR.

Kauli ya mkimbizi Kakuma kwamba bora elimu kuliko elimu bora ni ishara ya kiwango cha huduma hiyo-Onano

Utamaduni na Elimu

Mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR, Vivian Onano amezungumzia kile ambacho wakimbizi vijana wanataka kuhusu elimu baada ya kukutana nao na kuishi nao kwenye kambi ya Kakuma nchini Kenya.

Bi. Onano amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya ziara yake hiyo huko Kakuma ikiwa ni sehemu ya kampeni ya ufuatiliaji watu kwa kipindi cha mwaka mmoja katika harakati zao za kupata elimu, kampeni iliyopatiwa jina #EducationOnTheMove.

(Sauti ya Vivian Onano)

"Tulikuwa tunaongea na mmoja wao na akatania na kusema mara nyingi watu huzungumzia elimu bora lakini kambini wanachokijua ni bora elimu na kwa kauli hiyo pekee ni ishara muhimu ya kiwango cha elimu wanayoipata na ni dhahiri kwamba ni tofauti na mtu yeyote aliyoko katika nchi ya Kenya ambako wakimbizi hao wamo."

Na kwa mantiki hiyo Bi Onano ametoa pendekezo, "Kwa mantiki hiyo ni muhimu kuangalia kiwango cha elimu ambayo vijana wanapata kwasababu wana ndoto mbalimbali kwa mfano kuna ambao wanataka kuwa madakatari, wakulima au walimu lakini iwapo kiwango cha elimu wanachopata ni duni basi itakuwa vigumu kufikia ndoto zaoza."

Kampeni ya #EducationOnTheMove inalenga kutoa picha halisi ya upatikanaji wa elimu na imewaalika wahamiaji na wakimbizi kote ulimwenguni kuelezea panda shuka za kupata elimu ikiwa ni lengo namba nne la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.