Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa mgogoro wa Nicaragua, zaidi ya watu 60,000 wameikimbia nchi.

Wanicaragua wakiwa wanasubiri kufanya maombi ya hifadhi katika ofisi ya uhamiaji katika mji mkuu wa Costa Rica, San Jose (Agosti 2018)
UNHCR/Roberto Carlos Sanchez
Wanicaragua wakiwa wanasubiri kufanya maombi ya hifadhi katika ofisi ya uhamiaji katika mji mkuu wa Costa Rica, San Jose (Agosti 2018)

Mwaka mmoja wa mgogoro wa Nicaragua, zaidi ya watu 60,000 wameikimbia nchi.

Haki za binadamu

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbiazi UNHCR Liz Throssell amewaambia wana habari hii lemjini Geneva Uswisi kuwa inakadiriwa kuwa watu wapatao 62,000 wameikimbia Nicaragua na kusaka hifadhi katika nchi za jirani wengi wao kufikia 55,500 wakiingia Costa Rica kutokana na mazingira magumu nchini mwao tangu mwaka jana.

 

Mwezi Aprili mwaka jana wa  2018 nchini Nicaragua kulikuwa na maandamano ya nchi nzima dhidi ya mipango ya kufanyia mabadiliko mfumo wa hifadhi ya jamii ambapo zaidi ya watu 280 walipoteza maisha na maelfu walijeruhiwa.

Katika mtiririko mkubwa wa wakimbizi na wengi wao wakiepuka kuonekana, mara nyingi wakitembea kwa saa nyingi katika katika mazingira magumu, kwenye joto kali, fukuto n ahata hatari ya kupata malaria. Awali ilikuwa watu watu wazima waliokuwa wakivuka mpaka lakini sasa familia wakiwemo watoto wadogo wanakimbia.

Kwa mujibu wa mamlaka za uhamiaji za Costa Rica, hadi kufikia Machi 2019, takribani wanicaragua 29,500 walikuwa wamefuata utaratibu rasmi wa kuomba hifadhi. Mapokezi yakiwa tayari yamezidi kiwango, wako wengine 26,000 ambao wanasubiri maombi yao kupitishwa.

Miongoni mwa wale wanaoomba hifadhi wamo wanafunzi, waliokuwa wafanyakazi wa serikali, viongozi wa upinzani, wanahabari, madaktari, wanaharakati wa haki za binadamu na wakulima.

Bi Throssel ameeleza kuwa, “Idadi kubwa ya wale wanaofika wana uhitaji mkubwa wa huduma za kiafya, msaada wa kisaikolojia, malazi na chakula.”

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na shirika la Haki la Inter-American, IACHR, wameeleza wasiwasi wao kuhusa hali inayotetereka huko Nicaragua tangu mwezi Aprili 2018, kukiripotiwa ukikukwaji mkubwa dhidi ya wale walioshiriki katika maandamano ya kuipinga serikali na wale waliowasaidia.

Kumbukumbu ya mwaka mmoja ya maandamano hayo ikikaribia baadaye katika juma hili, kamishina mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR Michelle Bachelet hii leo amesema kuwa serikali ya Nicaragua inapaswa kuhakikisha vikosi vyake vya usalama vinawapa wananchi haki yao ya kukusanyika kwa amani na kueleza maoni yao kwa uhuru.

“Nina wasiwasi kuwa maandamano ambayo yamepangwa kufanyika baadaye wiki hii yanaweza kuchochea vurugu nyingine. Ukiukwaji wa miaka iliyopita ni pamoja na kuwanyanyasa na kuwashambulia viongozi wa wanafunzi, wanaharakati wa haki za binadamu, wana habari na wakosoaji wengine wa serikali. Mamlaka pia zimebana vyombo vya habari, zimezuia maandamano, pia kuna matumizi ya nguvu zilizipindukia na polisi kuwakamata watu bila kufuata utaratibu.” Bachelet amesisitiza.