Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtoto ana haki ya kupatiwa fursa achanue kadri atakavyo- Dua Lipa

Muugaji mkono wa shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Dua Lipa (kulia) akiwa amemtembelea mkimbizi wa Syria, Yazee Abdl El Eter kwenye kambi yao huko Beirut, Lebanon.
© UNICEF/UN0299659/Modola
Muugaji mkono wa shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Dua Lipa (kulia) akiwa amemtembelea mkimbizi wa Syria, Yazee Abdl El Eter kwenye kambi yao huko Beirut, Lebanon.

Kila mtoto ana haki ya kupatiwa fursa achanue kadri atakavyo- Dua Lipa

Msaada wa Kibinadamu

Mwanamuziki mashuhuri na muungaji mkono wa shughuli za shirika la Umoja wa Mataif ala kuhudumia watoto, UNICEF Dua Lipa ametembelea watoto wakimbizi wa kipalestina waliopatiwa hifadhi nchini Lebanona na kupata fursa ya kuzungumza nao kufahamu ndoto na matarajio yao. 

Mjini Beirut, nchini Lebanon, Dua Lipa, ametembelea wanafunzi katika shule inayoendeshwa na shirika la kiraia liitwalo Najedh kwenye kambi hii ya Burj el Barajneh ya wakimbizi wa kipalestina.

Lebanon inahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni moja kutoka Syria wakiwemo watoto wapatao Laki Tano, wengi wao wakiwa wamekumbwa na ukatili na bado wanahaha kupata huduma za kutosha kama elimu au afya.

Akiwa hapa Dua anashiriki nao michezo kama vile mpira wa kikapu, kisha anatembelea darasa la urembo ambapo wanafunzi wa kike wanajifunza jinsi ya kupaka urembo.

Kutoka hapa anaongozwa na kuvinjari ndani ya kambi ya muda ya wakimbizi wa Syria na kushuhudia miundombinu ya kijamii kama vile vyoo visivyo rafiki kwa wasichana na watoto.

Watoto wanampokea kwa mashamsham, tabasabu dhahiri licha ya machungu wanayokumbana nayo ugenini, nyumbani nako hawafahamu watarejea lini.

Dua anapata fursa ya kuzungumza nao mmoja akimweleza kuwa ndoto yake ni kuwa daktari..

Ndani ya hema moja anakutana na mama mzazi wa Yazee, ambaye anatoa shukrani kwa kuona jinsi Dua ameguswa na hali zao akisema ana matumaini kuwa anaweza kubadili hali zao.

Dua ambaye ni mzaliwa wa Uingereza, wazazi wake wakiwa ni wahamiaji kutoka Albania baada ya ziara  yake hiyo ya kwanza ya UNICEF anasema, “nahisi kuwa nina bahati kwa kupatiwa fursa hii hususan kwa kuzingatia natoka familia ya wahamiaji. Kuzaliwa Uingereza na kuweza kuishi ndoto yangu, kwasababu nilikuwa na ile fursa na naamini kila mtoto anapaswa kuwa na fursa hiyo pia. Kuweza kuwepo kwenye eneo ambalo watachanua na kuwa watu bora zaidi.”

TAGS: Dua Lipa, Lebanon, Syria, Palestina