Notre Dame ikiteketea,UN yapaza sauti
Mjini Paris, Ufaransa wingu zito la moshi limetanda angani wakati huu ambapo kanisa kuu la kale mjini humo, Notre Dame linateketea kwa moto.
Vyombo vya habari vinaripoti kuwa moto huo ulioanza saa 12.30 jioni kwa saa za Ufaransa leo Jumatatu tayari umeporomosha mnara mkuu wa kanisa hilo lililojengwa kuanzia mwaka 1163 hadi mwaka 1345.
Hadi sasa askari wa zimamoto wanaendelea kuhaha kudhibiti moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika.
Horrified by the pictures coming from Paris with the fire engulfing Notre Dame Cathedral - a unique example of world heritage that has stood tall since the 14th century. My thoughts are with the people and government of France. https://t.co/KnLegnlRFH
antonioguterres
Kufuatia tukio hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, “ nimeshtushwa na picha zinazotoka Paris zikionesha moto unateketeza kanisa kuu la Notre Dame, mfano wa kipekee wa urithi wa dunia ambao umesimama imara tangu karne ya 14.”
Katibu Mkuu amesema kuwa fikra zake hivi sasa zipo na wananchi na serikali ya Ufaransa.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO Audrey Azoulay amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa hisia kubwa zimezingira watu wanaoshuhudia kuungua moto kwa kanisa hilo ambalo UNESCO ililiorodhesha kama urithi wa dunia mwaka 1991.
“UNESCO inafuatilia kwa karibu hali ilivoy na ikon a mshikamano na Ufaransa ili kulinda na kukarabati urithi huo wa aina yake,” amesema Bi.Azoulay.