Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makombora na mashambulizi kutoka angani yazidi kuua raia mjini Tripoli na viungani

Khalid, mwanafuzi mwenye umri wa miaka 19 kutoka Ajdabiya, amelazimika kukimbia nyumbani kwao kutokana na mashambulizi na mapigano mjini humo.
UNHCR/P. Moore
Khalid, mwanafuzi mwenye umri wa miaka 19 kutoka Ajdabiya, amelazimika kukimbia nyumbani kwao kutokana na mashambulizi na mapigano mjini humo.

Makombora na mashambulizi kutoka angani yazidi kuua raia mjini Tripoli na viungani

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Libya idadi ya watu waliouawa tangu kuanza kwa mapigano kwenye mji mkuu Tripoli tarehe 6 mwezi huu wa Aprili imeongezeka na kufikia 48.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA imesema miongoni mwa hao 48 waliouawa hadi sasa ni pamoja na raia 13 huku ikiongeza kuwa idadi inatarajiwa kuongezeka kutokana na mashambulio kutoka angani na makombora yanayoendelea kuporomoshwa.

Idadi ya raia waliokimbia makazi yao nayo imeongezeka na kufikia zaidi ya 18,000, limesema shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM huku likifafanua kuwa miongoni mwao hao, 2500 wamekimbia makazi yao ndani ya saa 24 zilizopita.

Hata hivyo IOM inasema maelfu ya raia bado wamenasa kwenye maeneo yenye mapigano kwenye viunga ya kusini mwa Tripoli na kwamba licha ya kuomba msaada waweze kuondoka bado hawajaweza kufanya hivyo.

Hospitali nazo zilizopo kwenye maeneo ya mapigaon zinaendelea kupokea wagonjwa kila uchao mashambulizi yakikwamisha harakati za madaktari na magari ya wagonjwa kufikia wahitaji.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limethibitisha kushambuliwa bohari yake huko Ain Zara, bohari ambayo inahifadhi zaidi ya nakala milioni nne za vitabu vya kiada vya shule za sekondari na msingi.

Watoa huduma za misaada ya kibinadamu wanahofu kuwa kuendelea kuporomoshwa kwa mashambulizi kutoka angani na makombora mazito kwenye maeneo ya mijini kunaathiri miundombinu ya kiraia.

OCHA imenukuu jamii ya usaidizi wa kibinadamu ikisihi pande zote kwenye mzozo wa Libya zizingatie wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa na zijizuie kushambulia shule na vituo vya afya sambamba na wafanyakazi.