#Kwibuka25 : Rwanda ilikuwa ni funzo lakini funzo hilo liwe na mchango- Manusura wa mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi

12 Aprili 2019

Kumbukizi ya miaka 25 tangu ya mauaji ya kimbari dhidi ya wa Tutsi nchini Rwanda yamefanyika hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani  hii leo Ijumaa yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu Antonio Guterres na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo maalum kwa Katibu Mkuu Guterres amesema katika moja ya kurasa zenye giza zaidi katika historia ya binadamu, takriban watu milioni moja waliuawa wengi wakiwa ni watutsi lakini pia wahutu wenye msimamo wa wastani na wengine waliopinga mauaji hayo, ukatili huo ukifanyika kwa kipindi cha miezi mitatu.

Bwana Guterres amesema katika siku hii dunia inawaenzi waliouawa na kutafakari kuhusu mateso ya manusura akisema kuwa Umoja wa Mataifa unasimama pamoja na Rwanda na kwamba, “lakini tafakari yetu kuhusu msiba wa Rwanda unapaswa kwenda mbali zaidi ya nchi moja au tukio moja katika historia, ni lazima tutathmini hali ya sasa.”

Katibu Mkuu amesema, “kumbukizi ya ya leo inatoa fursa kwetu sisi kwa mara nyingine kupaza sauti dhidi ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na mifumo mingine ya kutovumiliana ikiwemo ubaguzi wa kijamii na kikabila, chuki dhidi ya waislamu na wayahudi.”

 Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres ametoa wito kwamba pale uovu huo unatokea, maovu hayo yanapaswa kugunduliwa, kukabilianwa nayo na kuyasitisha ili kuzuia kusababisha kama yalivyofanya awali ukatili uliochochewa na chuki na mauaji ya kimbari.

Viongozi wa kisiasa na kidini wana dhima kubwa kuepusha mauaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akihutubia baraza kuu wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi.
UN News/Elizabeth Scaffidi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akihutubia baraza kuu wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi.

Guterres ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, kidini na vyama vya kiraia kukataa hotuba za chuki na ubaguzi na kufanya kazi kuzuia vichochezi vinavyodunisha maridhiano ya kijamii na kuweka mazingira ya chuki na kutovumiliana.

Ameongeza kwamba uovu “umekita mizizi katika jamii zetu” lakini pia uwezo wa kuelewana, wema, haki na maridhiano na hio ndio funzo kubwa kutoka kwa kilichoikumba Rwanda.

Pongezi kwa Rwanda kwa kuwa mfano

 Guterres ameipongeza Rwanda kwa kuibuka kutoka mauaji hayo na hatua ilizopiga ikiwemo kama mchangiaji wa walinda amani kwa ajili ya operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, Rwanda pia imekumbatia maendeleo endelevu ya ulinzi wa mazingira, na kwamba baada ya kupitia ukatili wa kijinsia, wanawake wanashikilia asilimia 60 ya viti bungeni, “mfano mwingine ambao Rwanda inaweza kuigwa na dunia.”

Rais Kagame aahidi Rwanda kuendelea kuchangia zaidi walinda amani

Waliokusanyika kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 25 tangu mauaji ya kimbari ya Rwanda.
UN News/Elizabeth Scaffidi
Waliokusanyika kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 25 tangu mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Naye rais wa Rwanda, Paul Kagame katika tukio la leo la kumbukizi ya mauaji ya kimbari hayo amesema, “kumbukizi ni kitendo cha kuzuia. Wakati mauaji ya kimbari hayafanyiki yanachukua muundo wa kutokubali na kupuuza. Kukataa ni msimamo wa mauaji ya kimbari.Kukabiliana na hisia za kutokubali ni muhimu kwa ajili ya kuvunja mnyororo na kuzuia marudio ya kitendo hicho. Ni kwa muktadha huo ndipo Baraza Kuu kwa kauli moja lilipitisha mwaka jana tamko, “mauaji ya kimbari”dhidi ya watutsi na kwa hilo. “ninatoa shukrani za dhati.”

Rais Kagame ameongeza kuwa, “kwa miaka mingi, Rwanda imekuwa katika nchi tano za juu kuchangia walinda amani kwa ajili ya shughuli za ulinzi wa amani na tunadhamiria kuendelea na hilo, lakini Rwanda sio tu inachangia wanajeshi na polisi, tunachukua wajibu huo kutokana na misingi tuliyoipata kutokana na historia yetu. Kama taifa ambalo wakati mmoja lilisalitiwa na jamii ya kimataifa, tumejizatiti kutekeleza wajibu wetu na kufanya kazi na wengine kuimarisha mambo katika siku zijazo.”

Manusura naye apaza sauti

Mmoja wa manusura wa mauaji ya kimbari Rwanda Esther Mujawayo alipata fursa ya kuzungumza kwenye hafla hiyo akisema, “ninawaambia kwamba, ni kweli tunaweza kujenga upya maisha, licha ya kila kitu, licha ya machungu. Unaweza kuwa hai lakini ili kufanikisha hilo ni lazima kila mtu aweke juhudi.” 

Bi. Mujawayo ameongeza kwamba, “ninatoa changamoto hii, tuna funzo, Rwanda ilikuwa ni funzo lakini ebu funzo hilo liwe na mchango.”

 Kwa upande wake rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa amesema, “natamani tungewaenzi waliofariki miaka 25 iliyopita kwa kushinda chuki, kutovumiliana, ugaidi na ukatili wa mauaji. Lakini doa ndani ya nyoto zetu linasalia, kumekuwa na majanga mengi tangu wakati huo.”

Ameongeza kuwa, “wakati tukiwasha mishumaa asubuhi hii, hebu tuimarishe juhudi zetu za kufikia ahadi yetu ya “isifanyike tena.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter