Majaji wa ICC watupilia mbali ombi la Bensouda la kuchunguza Afghanistan

Makao makuu ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC huko The Hague, Uholanzi
UN /Rick Bajornas
Makao makuu ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC huko The Hague, Uholanzi

Majaji wa ICC watupilia mbali ombi la Bensouda la kuchunguza Afghanistan

Haki za binadamu

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC hii leo kwa kauli moja wametupilia mbali ombi la mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Fatou Bensouda ya kutaka kufanya uchunguzi dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni  vitendo vya uhalifu wa kivita na kibinadamu vilivyofanyika nchini Afghanistan.

Bensouda alisaka ombi hilo ili aweze kuchunguza vitendo hivyo vinavyodaiwa kufanyika wakati wa vita nchini humo tangu tarehe mosi mwezi Mei mwaka 2003 sambamba na vitendo kama hivyo vilivyofanyika katika mataifa mengine wanachama wa mkataba wa Roma tangu tarehe1 Julai mwaka 2002.

Tarehe 20 mwezi Novemba mwaka 2017, Mwendesha mashtaka huyo aliomba kibali kwa majaji hao ili aanzishe uchunguzi huo ambapo hii leo majaji  hao Antoine Kesia-Mbe Mindua, Tomoko Akane na Rosario Salvatore Aitala wamesema baada ya kupitia kwa kina ombi hilo wameona ingawa kuna msingi wa uchunguzi lakini muda umepita.

Majaji hao kwenye uamuzi wao wamesema, “muda  umepita tangu kuanza kwa uchunguzi wa awali mwaka 2006 na mazingira ya kisiasa nchini Afghanistan yamebadilika tangu wakati huo. Halikadhalika mwendesha mashtaka amekosa ushirikiano na hali ya ushirikiano inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo uchunguzi huu utaanzishwa na hivyo kuweka fursa finyu ya kuufanikisha.

Majaji hao wamesema “ni vyema kuelekeza rasilimali hizo za mahakama kwenye shughuli ambazo zina fursa kubwa zaidi ya kufanikiwa.”

Hitimisho la majaji hao ni kwamba uchunguzi kwa suala la Afghanistan kwa sasa hautakuwa na maslahi yoyote ya haki na hivyo wamepinga ombi la mwendesha mashtaka la kutaka kusonga mbele na uchunguzi.

Tarehe 5 mwezi huu wa Aprili, Marekani ilitangaza kufuta kibali cha kuingia nchini humo cha Bi. Bensouda kutokana na nia yake ya kuanzisha uchunguzi huo Afghanistan.