CERF yatoa dola milioni 125 kwa maeneo yaliyoathiriwa na mizozo, Tanzania, DRC na Uganda zimo.

11 Aprili 2019

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, Mark Lowcock ameidhinisha kiasi cha dola za kimarekani milioni 125 kutoka katika mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF kwa ajili ya kusaidia kwenye maeneo 13 ya mizozo ambayo hayana ufadhili wa kutosha (UFE).

Kiwango hiki cha fedha ni kikubwa zaidi kuwahi kutolewa katika mfuko wa CERF na kimewezekana kutokana na kuongezeka kwa ukarimu wa wafadhili kwa mfuko huo.

Bwana Lowcok amsesema, “fedha hizi kutoka CERF ni mwokozi wa maisha kwa mamilioni ya watu ambao wamekwama katika mizozo kote duniani ambaako kiwango cha mateso kinatia wasiwasi lakini ufadhili umekuwa ukisalia chini. Bila ufadhili huu, maji safi, malazi, ulinzi, lishe, msaada wa chakula na mahitaji mengine muhimu vinaweza visiwafikie watu kwa wakati katika kipindi ambacho wana uhitaji.”

Ameongeza kuwa kiasi hiki cha fedha kitaufanya Umoja wa Mataifa na wadau wake wa masuala ya kibinadamu kuweza kuendeleza operesheni zake za misaada kwa zaidi ya watu milioni 9 katika nchi za Cameroon, Chad, Colombia, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Djibouti, Haiti, Honduras, Madagascar, Niger, eneo la Palestina lililokaliwa (oPt), Tanzania, Uganda na Ukraine.

Zaidi ya wanawake na wasichana nusu milioni watapokea msaada katika upande wa unyanyasaji wa kijinsia na takribani wengine 400,000 watasaidiwa katika upande wa afya ya uzazi. Jumala ya dola milioni 24 zitaelekezwa katika miradi ya kusaidia zaidi ya watu milioni mbili wanaohitaji ulinzi wa haraka katika nchi 10. Zaidi ya dola milioni 7 zitasaidia juhudi za elimu kwa zaidi ya watoto 150,000 nchini Cameroon, Chad, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Madagascar, Niger, Palestina na Ukraine. Zaidi ya watu 350,000 wenye ulemavu kote katika nchi hizo watanufaika kutoka katika ufadhili wa CERF. 

“Ninazishukuru nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa na wafadhili ambao wamefanikisha hili na ninahamasisha ukarimu zaidi wa kufadhili mipango yetu mingine ya misaada.” Bwana Lowcock amesema.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter