Licha ya mapigano Libya, WHO yaendelea kupeleka vifaa vya matibabu

Picha ya maktaba ikionesha gari la dharura baada ya mashambulizi katika wizara ya mambo ya nje ya Libya mjini Tripoli.
UNSMIL
Picha ya maktaba ikionesha gari la dharura baada ya mashambulizi katika wizara ya mambo ya nje ya Libya mjini Tripoli.

Licha ya mapigano Libya, WHO yaendelea kupeleka vifaa vya matibabu

Msaada wa Kibinadamu

Wakati mapigano yakishamiri kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli na viunga vyake, huku idadi ya manusura ikiongezeka hadi mamia, shirika la afya ulimwenguni, WHO limechukua  hatua ya haraka kupeleka vifaa vya matibabu vinavyohitajika zaidi.

Mwakilishi wa WHO nchini Libya, Dkt. Syed Jaffar Hussain amesema pamoja na vifaa hivyo vya matibabu kwa ajili ya hospitali za mashinani na magari ya wagonjwa, wamepeleka pia timu za dharura za wataalamu wa afya zitakazosaidia  hospitali zilizo karibu na uwanja wa mapigano.

Yaelezwa kuwa makombora mazito na milio ya risasi imekuwa ni jambo la kawaida mjini Tripoli kwa siku 6 sasa ambapo watu 56 akiwemo dereva wa gari la wagonjwa na madaktari 2 wameuawa na raia wengine 266 wamejeruhiwa.

Maelfu ya watu wamekibia makazi yao ilhali wengine wamenasa katikati ya maeneo ya mapigano, hospitali zilizo nje na ndani ya mji wa Tripoli zikipokea wagonjwa kila uchao.

Dkt. Hussain amesema pamoja na kupeleka vifaa vya matibabu kwenye hospitali za mjini Tripoli, wametuma pia madaktari na vifaa vya kusaidia wagonjwa waliokumbwa na kiwewe kwenye hospitali ya Tarhouna, karibu na Tripoli na pia wanashirikiana na wadau wao kukidhi mahitaji ya wahamiaji na wakimbizi wa ndani.

Hata hivyo amesema kazi zinazofanywa na magari ya kuhudumia wagonjwa na timu za dharura zinakwamishwa na mashambulizi ya makombora ikiwemo kwenye maeneo yenye wakazi wengi, huku ukosefu wa mafuta ya petrol ukikwamisha azma yao ya kuwafikishia mahitaji ya kitabibu wahamiaji waliohama kutoka vituo ambamo walikuwa wanashikiliwa.

 “Hofu yetu ni kwamba mapigano haya yakiendelea kwa muda mrefu tutakuwa na manusura wengi, vifaa vyetu vya tiba vitamalizika na miundombinu ya afya itakuwa imesambaratishwa, hivyo tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa ihakikishe inatupatia fedha zaidi,” amesema Dkt. Hussain.

Mapigano  yalianza upya nchini Libya Jumamosi iliyopita na kusababisha hata kuahirishwa kwa mjadala wa kitaifa uliokuwa ufanyike kwa siku tatu nchini humo kuanzia tarehe 14 mwezi huu ili kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka minane sasa.