Hewa chafuzi zinasababisha bahari kukosa oksijeni

11 Aprili 2019

Uchafuzi wa mazingira utokanao na hewa chafuzi hivi sasa umebadili maisha ya viumbe vya bahari ikiwemo samaki waliozoeleka kuishi kwenye vina vya chini zaidi ya bahari.

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP linanukuu wanabaiyologia wa viumbe vya bahari wakisema uchafuzi huo unasababisha kukosekana kwa hewa ya oksijeni kwenye vina vya chini vya bahari na hivyo kusabaisha samaki kama Jodari na Chuchunge ambao awali walipatikana kwenye kina cha hadi mita 200 ndani ya bahari hivi sasa kuchomoza juu ya bahari ili kuvuta hewa hiyo.

Mjumbe maalum wa UNEP kwa ajili ya bahari, Peter Thomson amesema viwango vya joto vya maji ya bahari vimeondoa oksijeni kwenye maji na hivyo kufanya vigumu kwa samaki hao kuvuta pumzi ndani ya maji.

Amesema kama hiyo haitoshi, kadri dunia inavyopata joto zaidi joto la maji ya bahari nalo linaongezeka.

“Iwapo unafikiria kuhusu ongezeko la joto la maji ya bahari, fikiria pia ongezeko la kina cha maji ya bahari, kuharibika kwa matumbawe na kiwango cha aside kwenye maji ya bahari,” amesema Thomson.

Ameongeza kuwa kwa mantiki hiyo inakuwa vigumu kwa samaki wenye magamba kuishi kwenye bahari.

Kwa mujibu wa Thomson, hali ni mbaya zaidi ya hewa chafuzi kama ile ya ukaa kwa sababu katika  mijadala kuhusu masuala ya uchafuzi bahari, athari za hewa hizo hazijapatiwa msisitizo kama ilivyo uchafuzi wa taka za plastiki kwa sababu hewa hazionekani.

Amenukuu ripoti ya shirika la hali ya hewa duniani isemayo kuwa asilimia 90 ya hewa chafuzi inaishia baharini.

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima kupatia kipaumbele taarifa hizo kwasababu kila pumzi ya pili ya oksijeni inayovutwa na binadamu inatokana na oksijeni iliyozalishwa na kiumbe cha bahari.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter