Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yaadhimisha miaka 100 tangu kuasisiwa kwake

ILO yaadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa.
ILO
ILO yaadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa.

ILO yaadhimisha miaka 100 tangu kuasisiwa kwake

Masuala ya UM

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa hii leo limeadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa shirika la kazi ulimenguni katika hafla maalum iliyofanyika kwenye makao makuu ya umoja huo New York, Marekani wakati huu ambapo kuna mabadiliko makubwa katika mazingira ya kazi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema, “tunaishi katika nyakati zisizotabirika, kwenye misukosuko na mabadiliko ya kiteknolojia. Ubunifu kama vile akili bandia zitasaidia kuimarisha uchumi na kufikia malengo ya maendeleo endelevu lakini wakati huo huo, soko la ajira litakuwa na msukosuko; ajira nyingi zitabuniwa na wakati huo huo kazi nyingi zitaharibiwa. Mfumo mzima wa kazi utabadilika na vile vile uhusiano katik ya kazi mapumziko na shughuli zingine.”

Maadhimisho hayo ya miaka 100 yanaangazia mustakabali wa kazi ambapo katibu mkuu ameelezea hisia zake kwamba dunia haiku tayari kukabiliana na mabadiliko haya yatakayoathiri wengi.

Bwana Guterres kwa upande wake amesema ili kukabiliana na hali ijayo ni muhimu kuwekeza katika elimu. 

Aidha ameongeza kwamba sera za kulinda jamii za kisasa zinahitajikwa kwa ajili ya wale watakaothirika na mabadiliko ya kiteknolojia. Akiongeza, “tunahitaji kuchagiza serikali na wadau kuliko wakati wowote ule.”

Katibu Mkuu huyo amekaribisha wito wa  kamisheni ya mustakabali wa kazi ya ILO inayoongozwa na mwenyekiti rais wa Afrika Kusini na waziri mkuu wa Sweden kwa mfumo wake uanolenga binadamu na kuimarisha maswala ya jamii katika karne ya kidijitali na kusema, “ wakati uchumi wa kidijitali ukifanya operesheni duniani bila mipaka, kuliko wakati mwingine, taasisi za kimataifa ni lazima zichukue nafasi muhimu kwa ajili ya mustakabali wa kazi tunaoutaka.”

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umojawa Mataifa,Maria Fernanda Espinosa, amekumbusha kwamba zaidi ya watu milioni 40 wameathiriwa na mifumo ya utumwa wa kisasa na kwamba watu milioni 190 hawana ajira ikiwemo theluthi tatu ambao ni vijana.  "Watu milioni 300 walioajiriwa ni maskini kote ulimwenguni na nusu yao ni vijana. Aidha watu bilioni 2 wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi kwa kawaida bila ulinzi wa jamii," amesema Bi. Espinosa.

Ameongeza kuwa, “ni kwa muktadha huu ambapo tunapaswa kufikia lengo namba 8 la malengo ya maendeleo endelevu. Ajira bora iko kati kati ya juhudi zetu za kukabiliana na umasikini na ukosefu wa haki.” Ameongeza kuwa, “ni muhimu kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma, kuwezesha wanawake, vijana, walio wachache, jamii za watu wa asili na watu wanoishi na ulemavu.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder akihutubia baraza hilo amesema, maadhimisho ya miaka mia moja “ni fursa ya kutathmini umuhimu wa ILO na mustakabali wake.”

Bwana Ryder amesema “mazingira ya kazi yanapitia mabadiliko mengi ambayo yanatoa fursa kwa wengi na kwa wengine yanaibua hisia za wasiwasi na hofu.”

Mkuu wa ILO amehitimisha kwa kusema kwamba mustakabali wa ajira hautaongozwa na maendeleo ya kiteknolojia lakini kwa maamuzi ambayo tutafanya kwa ajili ya mustakabali wetu.

Kesho tarehe 11 mwezi Aprili ambayo ndiyo siku halisi ya kuasisiwa kwa ILO miaka 100  iliyopita baada ya Vita Vikuu vya kwanza ya dunia, kutafanyika maadhimisho sehemu mbalimbali duniani kuanzia Suva  na Lima, hadi Bangkok, New Delhi, Addis Ababa, Abidjan, Moscow, Paris, Washington, DC, New York, Buenos Aires na Geneva.