Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukitaka ushindani katika uchumi kesho, wekeza leo katika katika elimu ya awali ya watoto-UNICEF

Ikiwa serikali za leo zinataka vikosi kazi vyao viwe shindani katika uchumi wa kesho, wanahitaji kuanza kuwekeza katika elimu ya awali ya watoto-UNICEF
UNICEF/Tapash Paul
Ikiwa serikali za leo zinataka vikosi kazi vyao viwe shindani katika uchumi wa kesho, wanahitaji kuanza kuwekeza katika elimu ya awali ya watoto-UNICEF

Ukitaka ushindani katika uchumi kesho, wekeza leo katika katika elimu ya awali ya watoto-UNICEF

Utamaduni na Elimu

Ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF mjini New York Marekani imeonya kuwa zaidi ya watoto milioni 175, yaani nusu ya watoto wote wanaotakiwa kuwa katika shule za awali kote duniani, hawasajiliwa katika elimu ya awali au chekechea na hivyo wanakosa fursa ya uwekezaji muhimu na kukosa usawa kuanzia mwanzo.

Ripoti hiyo inasema katika nchi zaa kipato cha chini hali ni mbaya zaidi kwani ni mtoto mmoja tu kati ya watoto watano ambaye amesajiliwa katika masomo ya ngazi ya awali au chekechea.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Henrietta Fore anasema, “elimu ya awali au chekechea ni msingi wa elimu kwa watoto wetu. Kila hatua ya elimu inayofafuta inategemea mafanikio ya msingi huo. Lakini bado watoto wengi duniani kote wananyimwa fursa hii. Hii inaongeza hatari kwao kurudia darasa au kutoendelea na hiyo huwaweka kwenye vivuli vya wenzao ambao wamebahatika.”

Dunia iko tayari kujifunza

Ripoti hiyo ya kwanza ya aina yake kuhusu elimu ya awali duniani yenye jina “Dunia iliyo tayari kujifunza: kuipa kipaumbele elimu ya awali kwa watoto”, imeonesha kwamba watoto ambao wanajiunga na elimu ya wali angalau kwa mwaka mmoja wana uwezekano wa kujenga ujuzi wanaouhitaji ili kufanikiwa shuleni na wana nafasi ndogo ya kurudia darasa au kuacha shule na kwa hivyo wanakuwa na uwezo wa kuchangia katika jamii zenye amani na mafanikio na pia katika uchumi pindi wapoufikia utu uzima.

Aidha ripoti imeenda mbali zaidi na kueleza kuwa kipato au utajiri wa kaya, kiwango cha elimu ya mama na pia eneo la kijiografia ni moja ya vipengele muhimu vya mahudhurio ya elimu ya awali.

Baadhi ya matokeo muhimu ya utafiti:

Mchango wa umaskini: Katika nchi 64, watoto maskini wako chini mara saba kuliko watoto kutoka katika familia tajiri katika uwezekano wa kuhudhuria programu za elimu ya awali.

Athari ya migogoro: Zaidi ya theluthi mbili ya watoto wa umri wa kujiunga na elimu ya awali au chekechea wanaoishi katika nchi 33 ambazo zimeathiriwa na migogoro au majanga hawajaunganishwa katika programu za elimu ya awali kwa watoto.

Mzunguko wa elimu: Katika nchi zilizo na takwimu, watoto ambao wana mama zao waliohitimu masomo ya sekondari wako katika nafasi mara tano zaidi kujiunga na elimu ya wali kwa watoto kuliko watoto ambao mama zao wamehitimu elimu ya msingi tu au hawana kabisa elimu rasmi ya darasani.

Uwekezaji mdogo katika elimu ya awali ya watoto una matokeo mabaya katika ubora wa huduma ikiwemo upungufu wa walimu wenye ujuzi. Kwa pamoja, nchi zenye kipato cha chini na kile cha kati chini zina asilimia 60 ya watoto wenye umri wa kujiunga na elimu ya awali ya watoto lakini wana upungufu wa asilimia 32 ya walimu wa elimu ya awali.

Kwa ongezeko la idadi ya watu, kwa kufikiria kwamba mwalimu mmoja kwa wastani anatakiwa kuhudumia watoto 20, dunia itahitaji walimu wapya milioni 9.3 wa elimu ya awali au chekechea ili kufikia lengo la elimu ya awali kwa wote kufikia mwaka 2030.

“Ikiwa serikali za leo zinataka vikosi kazi vyao viwe shindani katika uchumi wa kesho, zinahitaji kuanza na elimu ya awali. Ikiwa tunataka kuwapa watoto wetu kitu bora katika maisha ili kufanikiwa katika uchumi wa utandawazi, viongozi wanatakiwa kutoa kipaumbele, na kuwekeza kisawasawa katika elimu ya awali.”

UNICEF inazisihi serikali kufanya angalau mwaka mmoja wa elimu bora ya awali kupatikana kwa wote hasa watoto walioko katika mazingira hatarishi na waliotengwa. Ili kufanya jambo hili kuwa halisi, UNICEF inazisihi serikali kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti zao za elimu kukuza elimu ya wali ya watoto na kuwekeza kwa walimu, ubora wa viwango na upanuzi wa usawa.