Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa kutatua changamoto za wakimbizi ni sasa:Grandi

Mtoto wa umri wa miaka 3 Laila Dalila Leon akiangalia mpaka kati ya Ecuador na Colombia waakati wa harakati za kuvuka.
UNICEF/UN0247721/Arcos
Mtoto wa umri wa miaka 3 Laila Dalila Leon akiangalia mpaka kati ya Ecuador na Colombia waakati wa harakati za kuvuka.

Wakati wa kutatua changamoto za wakimbizi ni sasa:Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Hakuna wakati mwingine muafaka wa kutatua changamoto kubwa zinazowakabili wakimbizi, waomba hifadhi, wakimbizi wa ndani na watu wanaofungasha virago kila uchao kwenda kusaka amani na mustakabali bora bali ni sasa.

Hayo ni kwa mujibu wa kamishina mkuu wa wakimbizi na mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Filippo Grandi akilieleza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu hali ya wakimbizi na changamoto zinazolighubika shirika hilo. Grandi amesema UNHCR inapitia mitihani mikubwa hivi sasa, mchanganyiko wa migogoro na vita vinavyosababisha wimbi la watu kutawanywa, changamoto mpya za kuomba hifadhi, pengo la ufadhili kati ya mahitaji ya kibinadamu na rasilimali na ongezeko la chuki dhidi ya wageni ni hatari sana.”

Ameongeza kuwa kwa upande wa wakimbizi kuna unyanyapaa mkubwa sana unaoendelea kwa wakimbizi na wahamiaji na hatua zilizokuwa zikichukuliwa awali zinazidi kupungua. Amesema ni vizuri kukumbuka huu ni mgogoro kwa nani “kwa mama mwenye watoto anayekimbia machafuko, kwa kijana anayekimbia vita, kwa serikali katika nchi masikini zinazofungua mipaka yake kwa maelfu ya wakimbizi kwa siku, kwao huu ni mgogoro”.

Hata hivyo amesema kusema mgogoro huu umeshindikana si sahihi kwani amesema anaamini kwa utashi wa kisiasa na hatua bora za kuukabili vinawezekana.

Grandi amesema kuna mambo matatu ambayo ni muhimu ambayo ni kuleta amani, kushughulikia changamoto za usalama na kuzisaidia nchi zinazohifadhi wakimbizi.

Ni vipi masuala haya yanatekelezeka

Mosi Grandi amesema ni kuondoa vikwazo vyote na kuvigeuza suluhu akitoa wito wa kushirikiana kutatua migogoro akitolea mfano Libya. Amesema karibu watu woto milioni 70 waliotawanywa ni kwa sababu ya vita, endapo migogoro hiyo ingezuiliwa au kutatuliwa, wimbi kubwa la wakimbizi lisingekuwepo. Amesisitiza ni muhimu kushughulikia vyanzo vya watu kukimbia kama vita na umasikini.

Pili ni kuzisaidia nchi zinazohifadhi wakimbizi. Akisema msichukulie kirahisi ukarimu wao, akiongeza kuwa anafahamu suluhu ya kisiasa ni mtihani lakini ni vyema kuwa na matarajio kwani changamoto ya watu kulazimika kufungasha virago itaendelea kuwepo na ni lazima kukukabiliana nayo. Katika hili amesema la muhimu ni kuongeza msaada kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi. Amesema asilimia 85 ya wakimbizi wote duniani wako katika nchi masikini  na ndiko kwenye migogoro na zinahitaji msaada na msaada huu sio tu wa kibinadamu lakini pia ni muhimu kwa kurejesha utulivu katika kanda nzima.

Tatu Grandi amesema suluhu ni changamoto lakini tunaweza kuchukua hatua kuondoa vikwazo vya kupatikana kwa suluhu. Amesema hivi sasa kuna shinikizo kubwa kwa wakimbizi kurejea makwao na wakimbizi wengine wako tayari kufanya hivyo lakini sehemu nyingi hali hairuhusu kwa wakimbizi hao kurejea.

Hivyo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushikamana ili kupata suluhu akisistiza kwamba “jamii zetu haziwezi kushamiri kama hazitomjumuisha kila mtu.”