Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano viungani Tripoli, ‘yapeperusha’ mazungumzo ya kuleta maridhiano nchini Libya

Tripoli, Libya picha ya maktaba ikionesha wananchi wakikusanya mizigo yao kwa ajili ya kuhama baada ya kupata vitisho kutoka kwa wapiganaji.
UNHCR/Tarik Argaz
Tripoli, Libya picha ya maktaba ikionesha wananchi wakikusanya mizigo yao kwa ajili ya kuhama baada ya kupata vitisho kutoka kwa wapiganaji.

Mapigano viungani Tripoli, ‘yapeperusha’ mazungumzo ya kuleta maridhiano nchini Libya

Amani na Usalama

Mkutano wa kitaifa uliokuwa unatarajiwa kufanyika nchini Libya ili kumaliza vita vilivyodumu nchini humo kwa miaka minane sasa umeahirishwa kutokana na mapigano yanayoendelea hivi sasa karibu na mji mkuu, Tripoli.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salamé, ametangaza hayo baada ya kulaani mashambulio ya jana kwenye  kiwanja cha ndege wa Meitiga yaliyofanywa na jeshi lililojitangaza la Libya, LNA. Kiwanja hicho ndio pekee ambacho kinatumiwa kwa ajili ya safari za kiraia.

Bwana Salamé ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa  nchini Libya, UNSMIL, amesema, hawawezi kufanya mazungumzo hayo katika mazingira ya sasa ya mashambulio ya makambora ya ardhini na angani akisema kwa kufanya hivyo itakwamisha azma ya wale wote ambao wamejitolea kusafiri kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ili kuwasilisha maoni yao uhuru na usalama.

Hata hivyo amesema kuwa yuko tayari kufanikisha mazungumzo hayo akisisitiza kuwa ameazimia yafanyike mapema iwezekanayo kwa kuwa yatakuwa ni fursa ya kihistoria.

Ameongeza kuwa atafanya kazi kwa uwezo wake wote ili mkutano huo ufanyike haraka iwezekanavyo pindi mazingira yanayotakiwa yatakapowezekana.

Mkutano huo wa kitaifa unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa ulikuwa ufanyike kwa siku tatu kuanzia tarehe 14 mwezi huu kwenye mji wa kusini-magharibi mwa Libya, Ghadames.

Matarajio ya mkutano huo yalikuwa ni kufikia makubaliano miongoni mwa vikundi mbalimbali vya kisiasa baada ya miezi ya majadiliano kuanzia ngazi ya chini ili hatimaye chaguzi za kidemokrasia ziweze kufanyika na kuunganisha wananchi wote na kisha Libya iweze kujikwamua kiuchumi.

Tayari ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR,  imetoa tamko lako kuhusiana na kile kinachoendelea Libya ikisema mashambulio yanayofanywa na LNA iliyo chini ya kamanda Khalifa Haftar vitendo vinavyofanywa dhidi ya raia na miundombini ya kiraia vinaweza kuwa uhalifu wa kivita.