Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko waua watoto wengine 14 na kuwajeruhi 16 wakiwa shuleni mjini Sana’a.

Picha ya maktaba ikionesha jengo lililoharibiwa kutokana na mapigano wakati wa mgogoro wa mwaka 2011 nchini Yemen
Giles Clarke/UN OCHA
Picha ya maktaba ikionesha jengo lililoharibiwa kutokana na mapigano wakati wa mgogoro wa mwaka 2011 nchini Yemen

Mlipuko waua watoto wengine 14 na kuwajeruhi 16 wakiwa shuleni mjini Sana’a.

Amani na Usalama

Mkurugenzi wa shirika la Umoj awa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kanda ya Mashariki ya kati na Kaskazini mwa Afrika, Geert Cappelaere kupitia taarifa iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Sana’a na Amman Yemen, amesema mlipuko uliotokea mjini Sana’a jana umewaua watoto 14 na kuwajeruhi 16 wakiwa shuleni na wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka tisa.

Bwana Cappelaere amesema kwa sasa hicho ndicho UNICEF imeweza kuthibitisha lakini idadi ya waliouawa na kujeruhiwa inaweza kuongezeka, “Watoto waliojeruhiwa vibaya, wengi wao wakiwa mahututi hivi sasa wako katika hospitali mjini Sana’a. Wengi wako chini ya umri wa miaka 9. Msichana mmoja aliyejeruhiwa amepoteza maisha jana asubuhi.”

Akifafanua kuhusu jinsi tukio hilo lilivyotokea, Bwana Cappelaere amesema mlipuko ulitokea karibu na shule mbili, na ilikuwa karibu kabisa na muda wa chakula cha mchana ambapo wanafunzi walikuwa darasani. Mlipuko ulipasua madirisha na kurusha vipande vya vioo ndani ya madarasa.

“Ni vigumu kufikiria hofu kubwa ambayo watoto waliipitia na pia wanavyojisikia wazazi kwa kufanya kile ambacho kila mzazi anapenda kufanya yaani kumpeleka mtoto wake shule. Kuua na kuwaumiza waatoto ni ukiukaji mkubwa waa haki za watoto.”  Amesema.

Geert Cappelaere amenukuliwa akisema kuwa mlipuko wa jana ni ukumbusho mwingine kuwa hata shule si mahali salama nchini Yemeni. Wengine wanakumbana na mashambulizi ya moja kwa moja na wengine wanatumika kwa manufaa ya kijeshi. Kwa watoto zaidi ya milioni mbili nchini Yemen hi leo, kwenda shule ni ndoto iliyoko mbali na mlipuko wa jana unaweza kuwavunja moyo wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni.

Katika saa 24 zilizopita, UNICEF imetoa msaada wa kuokoa maisha kwa watoto walioathirika na pia kwa familia zao ikiwemo kuwapatia msaada wa kisaikolojia, kugharamia upasuaji na matibabu mengine na pia kuwapatia msaada familia ili kusafiri kuungana na watoto wao katika maeneo wanakopatiwa matibabu.

Wakati huo huo, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffith akizungumzia tukio jingine lililosababisha vifo vya raia na wanafunzi katika eneo la Saewan mjini Sana’a mnamo tarehe 7 Aprili amesema amesikitishwa sana na anatuma salamu zake za rambirambi kwa wote walioathirika na janga.

Bwana Griffith amenukuliwa akisema, “ninazisihi pande zote kufaanya juhudi zote zinazowezekana kukomesha mateso kwaa raia na kuwaaruhusu watoto wa Yemen kukua katika amani na usalama. Suluhisho la kisisa litakaloshirikisha pande zote ndilo pekee litamaalizaa mzunguko wa vurugu na uharibifu.”

Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019, tayari zaidi ya watoto 400 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa sana nchini Yemen.