Diplomasia ya amani kuchagiza maendeleo endelevu Mashariki ya Kati- Guterres

6 Aprili 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani huko Jordan, amezungumza kwenye  jukwaa la kiuchumi duniani, WEF mjini Amaan na kusisitiza msimamo wa chombo hicho wa kutumia diplomasia ya amani ili kusongesha maendeleo endelevu na uwekezaji huko Mashariki ya Kati.

Jukwaa hilo la uchumi duniani kwa nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati ni la siku mbili na limeanza jana na linamalizika leo.

Bwana Guterres amesema diplomasia ya amani ni muhimu katika kutatua mizozo kama ule wa uwepo wa mataifa mawili yaani Israel na Palestina yakiwa na mipaka salama na inayotambulika huku Yerusalem ukiwa mji mkuu wa mataifa hayo mawili.

Amesema diplomasia ya amani imezaa matunda mathalani huko Tunisia ambako kumefanyika uchaguzi wa kwanza huru na wa kidemokrasia wa ngazi ya manispaa na kwamba kipindi cha mpito cha kidemokrasia kinaendelea.

Halikadhalika ametaja mazungumzo yake huko Misri na Imam Mkuu wa msikiti wa Al-Azhar ambao kwa pamoja walizungumzia pia umuhimu wa kusongesha kuheshimiana na stahamala, sambamba na harakati za Umoja wa Mataifa za kutokomeza kauli za chuki duniani.

Ukanda wa Fursa

Akimshukuru Mfalme Abdulla wa II wa Jordan na Malkia Rania Al Abdullah kwa kuwa wenyeji wa mkutano huo wa WEF na pia kuwa mabigwa wa amani, Bwana Guterres ameelezea Jordan kama msingi wa utulivu kwenye ukanda wa mashariki ya kati na nchi ambamo kwayo  ina fursa kubwa za kusongesha sekta binafsi.

Amesema ikiwa na idadi kubwa ya vijana, Jordan ni kichochea kikubwa cha utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kujumuisha sauti za vijana na iko katika mwelekeo wa kunufaika na mipango yake ya kujumuisha vijana.

Katibu Mkuu ameongea kuwa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, hayapaswi kuangaliwa tu kama maeneo ya ghasia bali pia ukanda wa fursa ambao ukipatiwa mwelekeo sahihi na usaidizi kutoka jamii ya kimataifa, unaweza kuchipuka na kuwa wa mfano.

Bwana Guterres amesema nchi kadhaa kwenye ukanda huo zimejumuisha matakwa ya raia wao kama vile hifadhi ya jamii, utawala bora na haki za binadamu, juhudi pia zimefanywa kutokomeza misimamo mikali, sambamba na kuondokana na ubaguzi wa kijinsia, ukatili wa majumbani na adhabu dhidi ya ukatili wa kingono.

Hata hivyo amesema juhudi zaidi zinatakiwa kuwezesha kiuchumi wanawake akisema kuwa usawa wa kijinsia una uwezo wa kuongeza pato la ndani la nchi hizo kwa dola trilioni 2.7 ifikapo mwaka 2025.

Shule za wakimbizi wa kipalestina haziwezi kufungwa.

Baada ya kuhutubia WEF, Katibu Mkuu alitembelea kambi ya Baqa’a, moja ya kambi za dharura zilizoanzishwa mwaka 1968 kwa ajili ya wakimbizi wa kipalestina na wakimbizi wa ndani ambao walikimbia ukingo wa magharibi wa mto Jordan na Gaza kutokana na vita vya waarabu na waisraeli vya mwaka 1967.

UNRWA
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres alipotembelea wanafunzi kwenye shule inayosimamiwa na UNRWA kwenye kambi ya Baqa'a nchini Jordan

Hii leo kambi hiyo inahifadhi takribani wakimbizi 120,000 wa kipalestina na ni kambi kubwa zaidi kaskazini mwa mji mkuu wa Jordan, Amman.
Akiwa kambini hapo amekutana na wafanyakazi na wanufaika wa misaada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wapelstina, UNRWA ambapo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufadhili shiriak hilo linalotoa misaada kwa wakimbizi hao wa kipalestina walioko Ukingo wa Magharibi, Gaza, Jordan, Lebanon na Syria.

Amesisitiza kuwa katu shule zinazohudumia watoto wakimbizi wa kipalestina hazitafungwa.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud