Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukiwa na mipango vijana hawatoenda kusaka hifadhi ughaibuni:CPD

Dkt. Paul Zebadia Mbano, mkurugenzi wa programu za afya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT,  akizungumza naIdhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.
UN News Kiswahili/ Grece Kaneiya
Dkt. Paul Zebadia Mbano, mkurugenzi wa programu za afya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT, akizungumza naIdhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Kukiwa na mipango vijana hawatoenda kusaka hifadhi ughaibuni:CPD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tatizo la uhamiaji ni moja ya changamoto kubwa katika kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 umesema mkutano wa 52 wa Umoja wa Mataifa wa Kamisheni ya idadi ya watu na maendeleo CPD ambao unafunga pazia hii leo. 

Suala hilo ni mada iliyoangaziwa kwa kina leo hii wakati huu ambapo mkutano huo ulioleta washiriki zaidi ya 125 wakiwemo mawaziri 60, ukizitaka nchi wanachama kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vijana wanapata fursa stahiki na vitu vitakavyowashawishi kutofunga safari za hatari kwenda ughaibuni kusaka mustakhbali bora.

Miongoni mwa washiriki katika mkutano huo ni Dkt. Paul Zebadia Mbano, mkurugenzi wa programu za afya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT,  akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa anafafanua changamoto ambazo Tanzania imekumbana nazo kwa ukarimu wake wa kupokea wageni.

Dkt. Mbando anasema, "Tanzania kwa kweli tumepokea watu wengi sana wakiwa wanakuja kama wakimbizi hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa, tumekuwa na watu kutoka Rwanda, kutoka Burundi, DRC ambao kwa kweli kinachowakimbizi kwao ni masuala ya kisiasa, masuala ya usalama, lakini kwa  upande mwingine wanavyokuja ni watu wanaohitaji huduma. Nchi inayowapokea inabeba mzigo mkubwa sana wa kufanya hivyo. Tuweke mazingira kwa watu wote waweza kujisikia kuwa pahala walipozaliwa panaweza kuitwa nyumbani. Kwenye upande wa vijana, wengi wanahamia nchi  nyingine kwa sababu ya ajira. Suala la ajira limekuwa ni suala la changamoto kwa nchi nyingi hasa Afrika. "

Soundcloud

Amegusia sakata la vijana kuuzwa kama utumwa lakini akasema, " Ni suala la kujiuliza tumekosea wapi?  Kwa sababu kwa nini kijana mwenye akili timamu aache familia  yake aende kufia kwenye maji baharini akiwa anajaribu kukimbia.  Anajikuta amekwama mahali kama Libya na anauzwa kama mtumwa. Nafikiri haya masuala na mengine mengi ambayo yamekuwa yanajadiliwa hapa ndani, kubwa lilionekana kwamba ongezeko la watu, lazima liwe na mipango, lakini ongezeko la vijana ambao ni wengi kwenye bara letu la Afrika, na vile vile pasifiki, tunavyokuwa tunao ni lazima tuwajibike kwenye kupanga jinsi vijana wanaweza kupata huduma wazohitaji."