Mashitaka dhidi ya viongozi wa ISIL yanatakiwa kuwa ya haki na ya kina.

4 Aprili 2019

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo hii mjini Geneva Uswisi ametoa wito kwa mamlaka nchini Iraq kuhakikisha mashitaka dhidi ya viongozi wa kundi la kigaidi la ISIL yafanyike katika mazingira ya uwazi na haki na yajumuishe ushiriki wa waathirika katika mchakato mzima wa kisheria.

Mjumbe maalumu kuhusu mauaji ya kiholela Agness Callamard amesema, “serikali ya Iraq inatakiwa kuchukua hatua sahihi kuhukumu makosa yaliyotendwa dhidi ya watu wa Iraq, ikiwemo yanayodaiwa kuwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na pia uhalifu wa kivita.”

Mnamo tarehe 30 ya mwezi Oktoba mwaka 2018, viongozi wa juu wa kundi la ISIL wakiwemo Wasyria wawili na raia wawili wa Iraq walihukumiwa adhabu ya kifo mjni Baghadad. Wanaume wanne walishitakiwa kutokana na uanachama wa kundi la ISIL chini ya sheria za kupambana na ugaidi za nchini Iraq ingawa taarifa zilizotolewa na watuhumiwa wenyewe zinaonesha kuwa wanaweza kuwa walishiriki, kushudia au kukiuka haki za binadamu na sheria za kibinadamu.

Mtaalamu huyo amsema, “Angalau, waendesha mashitaka wa Iraq walipaswa kuleta mashtaka ya ziada kutokana na kanuni ya adhabu ya Iraq, kama vile mashtaka ya mauaji, mateso au watu  kutoweka,  kwa madhumuni ya uwajibikaji.”

Aidha bi Callamard amesema makosa yanadaiwa kuwa yalitendwa na viongozi hao wa ISIL ndani ya Iraq na nje ya Iraq lakini hakuna mwathirika yeyote ambaye amehusishwa kwenye mwenendo wa kesi, au hata kuwasilisha ushahidi wao kama mashuhuda.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter