Skip to main content

FAO yazindua mwongozo wa kukabiliana na wadudu wavamizi

Mkulima katika shamba lake lililoshambuliwa na viwavi jeshi huko Namibia
FAO/Rachael Nandalenga
Mkulima katika shamba lake lililoshambuliwa na viwavi jeshi huko Namibia

FAO yazindua mwongozo wa kukabiliana na wadudu wavamizi

Ukuaji wa Kiuchumi

Kitendo cha wadudu wavamizi kuvamia miti na misitu na kuisambaratisha sasa kinafikia ukomo baada ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kupitisha mwongozo wa kuepusha vitendo hivyo.
 

Taarifa ya FAO iliyotolewa leo mjini Roma Italia na Beirut, Lebanon inasema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa wadudu waharibifu huharibu takribani eka milioni 35 kila mwaka ulimwenguni kote.
Wadudu hao wakiwemo mchwa hula miti ya thamani na ile ambayo binadamu si tu anaitegemea bali pia inamnufaisha.

FAO inasema hali ya uharibifu inakuwa mbaya zaidi pale wadudu ambao si wenyeji wa eneo hilo wanavamia bayonuai ambayo si ya kwao na kukosa wadudu wa kiasilia ambao wanaweza kukabiliana nao na kuwatokomeza.

Hata hivyo FAO inasema jawabu la sasa linatokana na kazi ya muongo mmoja uliopita ambapo wataalamu wamekusanya ufahamu wa kutosha wa kukabiliana na wadudu wavamizi waharibifu.

Wadudu hao wavamizi sasa wanapokwenda kwenye eneo la kuvamia watakutana na wadudu wa asili wa eneo lao wanalotoka “na hii imeonakan kufanya kazi kwa ufanisi katika udhibiti wa wadudu vamizi waharibifu,” imesema taarifa ya FAO.

FAO inasema mwongozo huo ukipatiwa jina “mwongozo wa kisasa wa kudhibiti wadudu waharibifu kwenye misitu iliyopandwa na misitu asili,” utatoa fursa kwa wasimamizi wa misitu kuandaa mipango bora na fanisi zaidi ya kukabiliana na wadudu waharibifu.

Akizungumzia mwongozo huo, Hiroto Mitsugi, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa FAO akiongoza idara ya misitu ametoa mfano wa mdudu Torymus sinensis, ambaye ni wa kundi la aina ya mchwa kutoka China, ambaye alisambazwa barani Ulaya baada ya mdudu wa asili hiyo kuleta uharibifu mkubwa wa kupunguza mavuno ya miti kwa asilimia 40.

Amesema hatua hiyo ilipunguza uharibifu kwa sababu aliua zaidi ya asiimia 75 ya wadudu hao waharibifu na kuacha mchwa asili pekee wa eneo hilo.

Mwongozo huo una maelekezo ya kukabiliana na wadudu waharibifu kadhaa ikiwemo wale wanaoshambulia minazi, miti ya mpira na mikaratusi.