Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wanaotumia tofauti kugawa watu wapingwe kwa nguvu zote- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikutana na Imam Mkuu wa msikiti wa Al Azhar Dkt. Ahmed El Tayeb kwenye msikiti wa Al- Azhar mjini Cairo Misri hii leo
UN- Misri
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikutana na Imam Mkuu wa msikiti wa Al Azhar Dkt. Ahmed El Tayeb kwenye msikiti wa Al- Azhar mjini Cairo Misri hii leo

Viongozi wanaotumia tofauti kugawa watu wapingwe kwa nguvu zote- Guterres

Utamaduni na Elimu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko ziarani nchini Misri amesema katika zama za sasa zilizogubikwa na misukosuko ni vyema kujikita katika kile kinachounganisha binadamu badala ya kile kinachowatofautisha.

Guterres amesema hayo alipotembelea msikiti wa Al Azhar mjini Cairo nchini Misri wenye historia ya zaidi ya miaka 1,000 sambamba na utamaduni, mafunzo na imani ya dini ya kiislamu.

Akizungumza huku akinukuu vifungu vya Qu’ran tukufu, Bwana Guterres ametaja misukosuko na mashambulizi dhidi ya waumini wa dini  ya kiislamu kuanzia huko New Zealand hadi mashambulizi dhidi ya wayahudi nchini Marekani.

Guterres amesema ingawa hivyo wamejitokeza watu wema kama ilivyo kwenye sura ya 34 ya Qu’ran tukufu isemayo,,

“Matendo mabaya na mema hayafanani. Epuka ubaya kwa kufanya jema na utaona yule ambaye awali alikuwa adui yako atakuwa rafiki mwema zaidi.”

Amesema ni katika nyakati hizi ngumu zenye mgawanyiko na chuki dhdiya waislamu, wageni, wayahudi, wenye imani na wasio na imani, ni lazima kushikamana na kulindana, akipongeza tamko la Imam Mkuu wa Al-Azhar

Sheikh Ahmed al-Tayeb, na Papa Francis la kushikamana kidugu.

Kwa mantiki hiyo amesema, "ni lazima tupinge na tuwakatae viongozi wa kidini na kisiasa ambao wanajinufaisha na tofauti. Lazima tujiulize ni kwa nini watu wengi wameenguliwa na wanachochewa na kauli za chuki za misimamo mikali dhidi ya wengine.

Amekumbusha kuwa ni kweli kuna watu wenye imani, tamaduni na historia tofauti lakini zaidi ya yote watu wote wanaunganishwa na  ubinadamu.