Wanawake hufanikiwa wakiwekeza katika sekta zinazohodhiwa na wanaume-Benki ya dunia

1 Aprili 2019

Benki ya dunia inasema wanawake barani Afrika wako katika mazingira ya kuingia katika kazi zisiso rasmi ikilinganishwa na wanawake wa maeneo mengi.

Biashara zinazomilikiwa na wanawake mara nyingi ziko katika masoko yaliyojaa watu wengi na wanamudu kuwaajiri wafanyakazi wachache, mauzo kidogo na ongezeko dogo la thamani.

Lakini utafiti mpya unaonesha kuwa wajasiriamali wa kike wanaweza kuanzisha makampuni makubwa na yenye faida wanapofanya kazi katika sekta ambazo kiasili zimehodhiwa na wanaume.

Video ya benki ya dunia inawaonesha baadhi ya wanawake wa Kiafrika waliovunja mwiko na kuingia katika sekta hizo mathalani za ujenzi na uzalishaji bidhaa.

Mariame Keita anamiliki kiwanda cha kufyatua matofali, na anasema,

(Sauti ya Mariame Keita)

“Kujifanyia kazi ni kitu kizuri kwasababu inakusaidia kujipatia mahitaji yako mwenyewe na familia yako.”

Wanawake wengi barani Afrika wako katika biashara zaidi za kuuza vitu kama nguo na siyo kazi kama vile usafirishaji, uzalishaji bidhaa na ujenzi.

Lakini utafiti wa Benki ya Dunia unaonesha kuwa wajasiriamali wa Kike wanaweza kupata faida kubwa katika kazi za sekta zilizohodhiwa na wanaume. Na makapumi yanayomilikiwa na wanawake ni makubwa kama yalivyo ya wanaume.

(Sauti ya Fatoumata Bintou Barry)

“Nilihamasika kuanzisha kampuni ya ujenzi, usafi, na malezi kwasababu ni sekta iliyohodhiwa na wanaume. Na nilijiambia, chochote mwanaume anachoweza kufanya, mwanamke anaweza kukifanya pia. Ninajisikia vizuri kuhusu kazi yangu.”

Mariame Keita anaongeza

(Sauti ya Mariame Keita)

“Katika miaka 10 ninataka kutengeneza nafasi zaidi ya 50 na niwaajiri wanawake katika biashara zangu. Lakini ninataka wanawake watambue kuwa pia wao wanaweza kufanya kazi zile ambazo kwa kawaida zinafanywa na wanawake.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter