Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yajiandaa kuwasaidia wakulima na wafugaji Msumbiji baada ya IDAI

Nyumba katika eneo la Nhangau ikiwa imesambaratishwa baada ya kimbunga Idai kuipiga Msumbiji.
UNICEF/DE WET
Nyumba katika eneo la Nhangau ikiwa imesambaratishwa baada ya kimbunga Idai kuipiga Msumbiji.

FAO yajiandaa kuwasaidia wakulima na wafugaji Msumbiji baada ya IDAI

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO  limesema linajiandaa kuzisaidia jamii za vijijini zilizoathirika na kimbunga IDAI nchini Msumbiji kufufua kilimo na masuala ya uvuvi.

Katika taarifa yake ya leo Ijumaa FAO inasema maisha ya wakulima na wavuvi katika nchi tatu za Kusini mwa Afrika zilizokumbwa na kimbunga IDAI ziko katika tishio kubwa na hasa jamii za Msumbiji .

FAO inasema kwa nchi ambayo asilimia 80 ya watu wake wanategemea kilimo, kuhakikisha uhai wa mifugo, kukarabati ardhi zilizoathirika na kufufua uzalishaji wa chakula itakuwa muhimu sana wakati maji ya mafuriko yanapokauka.

Kwa mujibu wa shirika hilo eneo kubwa la ardhi ya kilimo limeathirika ikiwa ni katika msimu wa mavuno ya mahindi ya mtama kati ya mwezi April-Mei. Hasara kubwa inatarajiwa katika majimbo ya Msumbiji ya Manica na Sofala ambayo kwa kawaida huchangia asilimia 25 ya nafaka zinazozalishwa kote nchini.

Kabla ya mafuriko Karibu nusu ya wakazi wa vijijini Msumbiji walikuwa na akiba ya mahindi, mihogo na maharagwe, lakini bila shaka mafuriko yameathiri asilimia kubwa ya akiba hiyo ya chakula na mbegu.

FAO inasema kabla ya zahma hii watu milioni 1.8 nchini Msumbiji walikuwa tayari wameathirika na kutokuwepo na uhakika wa chakula idadi ambayo sasa itaongezeka zaidi kutokana na kubainika kiwango halisi cha hasara iliyopatikana. FAO inaomba dola milioni 19 za awali ili kusaidia wakulima walioathirika zaidi katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa lengo la kufufua uzalishaji wa chakula , kuwasaidia jamii za wavuvi na wafugaji.

Mkakati wa FAO kwa ajili ya mifugo utajumuisha kuwahamisha baadhi ya mifugo hao, kuwahakikishia huduma za tiba ya mifugo na upatikanaji wa chakula. Limesema gharama halisi ya kuokoa maisha ya ng’ombe mmoja dhidi ya njaa na magonjwa ni takribani dola 50, wakati kununua ng’ombe wengine gharama itaongezeka na kufikia hadi dola 6000

Shirika hilo limesema wengine wanaohitaji msaada na ulinzi ni wavuvi, mali zao na miundombinu yao. Na hii ni muhimu hususani katika mji wa bandari wa Beira ambao unabeba sekta ya uvuvi na ndiko kulikuwa kitovu cha kimbunga Idai. Bandari ya Beira pia ndio bandari kuu kwa kuingiza zaidi ya tani milioni moja za ngano na mchele kila mwaka.