Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatutaki zahma nyingine katika maandamano yatarajiwayo kesho Gaza:McGoldrick

Waandamanaji wakitembea kuelekea katika eneo la kukusanyika katika uzio wa Gaza
UNifeed Video
Waandamanaji wakitembea kuelekea katika eneo la kukusanyika katika uzio wa Gaza

Hatutaki zahma nyingine katika maandamano yatarajiwayo kesho Gaza:McGoldrick

Amani na Usalama

Katika mkesha wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa maandamano ya Gaza mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya eneo linalokaliwa la Palestina Jamie McGoldrick amesema kipaumbele hivi sasa ni kuokoa maisha na kila mmoja anapaswa kuchukua hatua inavyostahili. 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi kufikisha ujumbe huo wa MaCGoldrick msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA bwana Jens Laerke amesema, “Vikosi vya Israel lazima vihakikishe kwamba hatua zake zinakwenda sanjari na wajibu wake wa kimataifa wa kutotumia njia za nguvu kwa kiasi kikubwa. Na mamlaka ya Hamas ni lazima izuie vitendo vya ghasia ambazo zitavuruga maanadanao ya amani na kila mtu lazima ahakikishe kwamba Watoto hawatodhuriwa.”

Ameongeza kuwa wanatarajia kwamba maandamano ya leo yamefutwa kwa matarajio na wito wa maandamano makubwa hapo kesho, na kwamba sababu ya kwa nini taarifa hii imetolewa leo na mratibu wa masuala ya kibinadamu ni kwa sababu yeye na jumuiya nzima ya kimataifa wanahofia kwamba watashuhudia zahma nyingine kubwa hapo kesho na wanataa kila kit una kila mtu afanye kila liwezekanalo kuepuka hilo. Amekumbusha kwamba, “mwaka jana kumekuwa na majeruhi na maisha ya watu wengi yamepotea kwenye Ukanda wa Gaza. Wapalestina 195 wakiwemo Watoto 40 wameuawa na vikosi vya Idrael hususan katika maandamano ya kila wikikaribu na uzio.”

Pia amesema Wapalestina karibu 29,000 wamejeruhiwa wakiwemo 700 kati yao ambao walijeruhiwa kwa risasi za moto, wahudumu watatu wa afya nao walipoteza maisha yao huku wengine zaidi ya 360 wakijeruhiwa.

OCHA imekumbusha kwamba kila anayehusika katika suala hili, ulinzi wa maisha ya watu na hususan watoto ni lazima upewe kipaumbele cha kwanza wakati wa yale wanayoyatarajia kuwa maandamano makubwa hapo Kesho.