Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshindi wa tuzo ya UN ya kijeshi ya jinsia mwaka huu ni Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga.

Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hafla iliyofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataiafa mjini New York Machi 29, 2019.
UN Photo/Cia Pak
Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hafla iliyofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataiafa mjini New York Machi 29, 2019.

Mshindi wa tuzo ya UN ya kijeshi ya jinsia mwaka huu ni Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga.

Masuala ya UM

Mlinda amani kutoka Brazili anayehudumu katika mpango wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya kati MINUSCA, Ijumaa hii anakabidhiwa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya kijeshi kwa mwaka 2019 katika utetezi wa masuala ya jinsia. 

Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga afisa wa jeshi la wanamaji la Brazil amekabidhiwa  tuzo hiyo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika mkutano wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ngazi ya mawaziri unaofanyika katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York Marekani.

Tuzo hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2016 inatambua mchango wa kujitolea na juhudi za mlinda amani mmoja mmoja katika kuendeleza malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na usalama.

Akihudumu kama mshauri wa kijeshi wa masuala ya jinsia katika Makao Makuu ya MINUSCA tangu mwezi April 2018, Luteni Kamanda Braga amesaidia kujenga mtandao wa washauri wa jinsia waliopata mafunzo ndani ya vikosi vya MINUSCA na pia alihamasisha matumizi ya timu mchanganyiko wa wanawake na wanaume kufanya doria za kijamii nchini kote.

Luteni Kamanda Braga ameeleza furaha yake baada ya kutangazwa mshindi wa mwaka huu, “nimefurahi kuchaguliwa. Mipango ya ulinzi ya Umoja Mataifa (kote duniani) inahitaji walinda amani wanawake zaidi ili wanawake wa maeneo husika waweze kuongea kwa uhuru kuhusu masuala yanayoathiri maisha yao.” 

 

Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga akihudumu katika kikosi cha MINUSCA huko CAR
MINUSCA/Hervé Serefio
Luteni Kamanda Marcia Andrade Braga akihudumu katika kikosi cha MINUSCA huko CAR

Na kuhusu shughuli zake,Braga anafunguka“Ninajihusisha na watu wa maeneo haya, na ninafanya mikutano na viongozi wa wanawake wa hapa ili kuwawezesha na kuwapa sauti, kuboresha ushiriki na kimsingi kwa uzoefu wangu hapa katika MINUSCA, wanawake wana hofu zaidi kuhusu amani kwa kuwa wana familia, kwa hivyo wanawake ni chanzo muhimu cha tarifa na kwa kutumia tarifa hizo tunaweza kutekeleza shughuli zetu na kuzuia vurugu.”   

Vikundi hivi vya ushirikiano vimeweza kukusanya taarifa muhimu za kusaidia mpango wa Umoja wa Mataifa nchini CAR kuelewa mahitaji ya kipekee ya ulinzi kwa wanaume, wanawake, wavulana na wasichana. Wamesaidia pia katika ujenzi wa pampu za maji karibu na vijiji, taa zinazotumia mwanga wa jua na kuendeleza bustani za jumuiya ili wanawake wasisafiri umbali mrefu kuhudumia mazao yao.

Luteni Kamanda Braga ambaye pia ni mwalimu wa zamani, amesaidia kuwafundisha na kukuza uelewa miongoni mwa wafanyakazi wenzake kuhusu tofauti za kijinsia ndani ya MINUSCA.