Athari za mabadiliko ya tabianchi duniani zinazongezeka:UN

28 Machi 2019

Dalili za wazi na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi zinazoongezeka kote duniani , zinatokea leo kwa kila nchi na hakuna aliye na kinga dhidi ya zahma hii  na hakuna kisingizio cha kukwepa kuchukua hatua kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio. 

Guterres amezungumza hayo leo katika ufunguzi wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kuongeza kuwa,“ni dhahiri kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatishia miongo ya hatua za maendeleo na kuweka hatarini mipango yetu yote ya maendeleo endelevu jumuishi. “

Ameongeza kuwa ni kweli kwamba kukabiliana na mabadilkiko ya tabianchi kunatoa fursa ya kuongeza kasi na kuchapuza maendeleo endelevu kupitia kuwa na hewa safi, kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya ya umma na itatoa usalamana ukuaji wa uchumi kwa mataifa yote.

UN/ MINUSTAH/Logan Abassi
Baada ya siku kadhaa za mvua katika maeneo ya kaskazini mwa Haiti, eneo hilo lilikumbwa na mafuriko na kusababisha watu kupoteza maisha na pia maelfu kukosa makazi (Novemba 2014)

 

Amehimiza kwamba hakuna ksingizo cha kuchukua hatua hasa ukizingatia madhara yanayoonekana kila konda ya dunia akitolea mfano kimbunga IDAI kilichoathiri Kusini mwa Afrika hivi karibuni, “Wakati wa kuchukua hatua ni sasa, tunahitaji hatua za pamoja zikijumuisha nchi zote, na tunahitaji zifanye kazi bega kwa bega na sekta binafsi na asasi za kiraia, mabadiliko ya tabianchi duniani yanatuma ujumbe wa wazi na vijana wanataka viongozi wachukue hatua kwa niaba ya vizazi vijavyo, nami nakubaliana na hilo.”

Akisisitiza wajibu wa kila mmoja katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwenye mkutano huo , Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa amesema “Sote tunaweza kupunguza mchango wetu wa hewa ukaa kila siku katika vyakula tunavyotumia, nguo tunazovaa, usafiri tunaochagua na taka tunazozalisha. Kwa hakika tunahitaji kubadilisha mfumo wa matumizi yetu , hii sio tu dunia iliyopungukiwa bali pia ya matumizi ya kupindukia. Na ukweli unaoumiza ni kwamba tani milioni 1300 za chakula hupoteza bure kila mwaka ili hali watu takrinban milioni 2000 wanakabiliwa na njaa na utapiamlo.”

Nayo ripoti mpya ya shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO iliyotolewa leo inasema majanga ya asili, ikiwemo mafuriko, vimbunga , joto la kupindukia, kuongezeka kwa kinga cha baharí  na matukio kama elnino vyote nvinaongezeka kutokana na mabadiliko haya ya tabianchi na hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi endapo hatua madhibuti hazitochukuliwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud