Vitendo vya uchokozi vinahatarisha usalama Mashariki ya Kati:Mladenov

26 Machi 2019

Wakati uhasama kati ya Israeli na Palestina ukiendelea kushuhudiwa, Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mchakato wa amani huko Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov ameelezea kuhusu hali mbaya inayoendelea ambako vitendo vya kigaidi, mashambulizi dhidi ya raia, makabiliano na waandamanji, uharibifu wa mali, kujengwa kwa makazi ya walowezi na janga la ufadhili ambavyo vimesababisha hali iliyokuwa mbaya kudorora zaidi.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumanne, bwana Mladenov amesema amesikitishwa na kuendelea kwa ukatili ambao unasababisha vifo vya Wapalestina na Waisraeli akisema, “matukio ya hivi karibuni katika ghuba ya Mashariki na Gaza ni ishara ya uhasama unaoendelea katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa na uwezekano wa mzozo kuongezaka.” Mratibu huyo maalum ameelezea wasiwasi wake kwamba huenda dunia ikashuhudia ukatili Gaza ambao madhara yake yatakuwa mabaya sana.

Bwana Mladenov amesikitikia kurushwa kwa makombora 104 kutoka ukanda wa Gaza kuelekezwa Israeli katika kipindi cha siku kumi zilizopita ambapo baadhi yalikamatwa na mfumo wa kukbailiana na makombora wa Israeli huku mengine yakisababisha uharibifu wa mali katika mji wa kusini wa Sderot na kupiga maeneo yaliyo wazi na moja likipiga nyumba na kusababisha majeruha kwa watu sababa wakiwemo watoto watatu.

Aidha Mladenov ameongeza kuwa hakuna sababu ya kuhalilisha vitendo vya kigaidi na hivyo ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa katika kulaani kitendo cha ulengaji wa makombora ya Hamas kuelekea Israeli ambavyo ameviita kama, “vitendo vya uchokozi” ambavyo “vinaongeza hatari ya kuongezeka uhasama na hatimaye kuathiri juhudi za pamoja za kuunga mkono watu wa Gaza na maridhiano ya Palestina.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN /Manuel Elias
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Bwana Mladenov amezingatia kwamba katika kujibu mashambulizi kwenye kipindi cha saa 48, vikosi vya Israeli vilirusha makombora 42 katika maeneo mbalimbali ya Gaza. Kwa mujibu wa vyombo vya habari mashinani, wapalestina saba walijeruhiwa na majengo kadhaa kuharibiwa ikiwemo ofisi ya kundi la msimamo mkali la Hamas linalosimamia Gaza.

Kwa kuzingatia hali inayoshuhudiwa sasa, bwana Mladenov amesihi Baraza la Usalama kutoa wito kwa pande husika katika mzozo kujizuia na vitendo kama hivyo.

Amekumbusha kwamba kufikia sasa hakuna hatua ambazo Israeli imechukua kusitisha shughuli za kukalia maeneo yanayoshikiliwa ya Wapalestina ikiwemo Mashariki mwa Jerusalem kama ilivyopendekezwa kwenye azimio la baraza la usalama namba 2334.

Bwana Mladenov amerejelea kauli yake kwamba ujenzi wa makazi katika maenep yanayokaliwa ya wapalestina ikiwemo mashariki mwa Jerusalem, hauna athari za kisheria na unajumuisha ukiukaji wa sharia ya kimataifa na inapaswa kusitishwa mara moja na kwa namna zote.

Njia ndogo kwenye kambi ya wakimbizi wakipalestina Gaza.
UN News/Reem Abaza
Njia ndogo kwenye kambi ya wakimbizi wakipalestina Gaza.

Mwakilishi maalum huyo ameelezea pia kwamba maamuzi ya Israeli kuchukua asilimia 6 ya mapato ambayo inapokea kwa niaba ya mamlaka ya Palestina na kukataa kwa mamlaka ya Palestina kuchukua kiasi cha mgao na sio mgao kamili kumesbabisha janga la ufadhili ambalo limekuwa na athari kwa wapalestina ikiwmeo kupunguzwa kwa asilimia 50 mshahara wa karibu theluthi mbili ya wafanyakazi wa serikali wa Palestina, kusitishwa kwa kupandishwa vyeo, kuajiri na nyongeza ikiwemo ya kununua mali na magari, “Isitoshe, malaka ya Palestina wanatarajia kukopa fedha kutoka kwa benki za nyumbani katika kipindi hiki hadi Julai ambayo itakuwa na athari katika uchumi wa Palestina na kupunguza uwezo wake wa kununua na kupunguza pato la taifa katika ghuba ya mashariki na Gaza.

Halikadhalika bwana Mladenov ameelezea kuendelea kusikitishwa na hali ya kutokuwepo hatua kuelekea kwa suluhu la mataifa mawili kwendana na amapendekeo ya maazimio ya Umoja wa Mataifa na makubaliano mengine.

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kuwepo, “uongozi na dhamira ya kisiasa kuchukua hatua stahiki katika kusitishwa kwa kuendelea kukaliwa maeneo hayo na kufikia amani ya kudumu,” akiongeza kuwa, “mpaka pale hilo litafikiwa kizazi kingine cha waisraeli na wapalestina huenda wakaishi maisha ya kutafuta amani isyopatikana.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter