Skip to main content

Watoto wanalipa gharama kubwa kwenye mgogoro wa Mali:UN

Mfanyakazi wa UNICEF akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ogossagou-Peulh, kilichoko Bankass katikati mwa Mali. Kiji hiki kilishambuliwa tarehe 23 Machi ambapo watu 150 waliuawa na wengine 2000 kukosa makazi kutokana na nyumba zao kuteketezwa kwa moto.
UNICEF
Mfanyakazi wa UNICEF akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ogossagou-Peulh, kilichoko Bankass katikati mwa Mali. Kiji hiki kilishambuliwa tarehe 23 Machi ambapo watu 150 waliuawa na wengine 2000 kukosa makazi kutokana na nyumba zao kuteketezwa kwa moto.

Watoto wanalipa gharama kubwa kwenye mgogoro wa Mali:UN

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesikitishwa na kughadhibishwa na kitendo cha watoto kuendelea kulipa gharama kubwa ya maisha yao kwenye mgogoro wa Mali. 

Kauli hiyo imefuatia shambulio la mwishoni mwa juma katika eneo la Bankass mjini Mopti  Mali ambapo watu zaidi ya 150 waliuawa, na 70 kujeruhiwa miongoni mwao wakiwa ni watoto. Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswisi hii leo msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac  amesema“tathimini ya awali inajieleza , theluthi moja ya waliokufa ni watoto na nusu ya waliojeruhiwa ni watoto, shule zinaendelea kutishiwa, hivyo vitisho dhidi ya Watoto ni dhahiri na watoto wanaendelea kulipa gharama kubwa ya mgogoro wa Mali .

Ameongeza kuwa watoto wengi waliojeruhiwa hivi sasa wamehamishiwa kwenye vituo vya afya kwa ajili ya matibabu na timu ya UNICEF kwa kushirikiana na wahudumu wengine wa kibinadamu na wizara ya afya ya Mali wako Mopti kwa ajili ya kutoa huduma ya kwanza na mahitaji mengine na tayari imeshapeleka vifaa vya dharura vya tiba ambavyo vitaweza kusaidia kwa muda wa miezi mitatu. Msaada mwingine wanaotoa ni wa kisaikolojia na ushauri nasaha kwa watoto wasio na walezi au wazazi.

Kwa upande wake ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema mashambulizi hayo ya kuwalenga watu kutokana na kabila au jamii ambayo ni ya Fulani ni ukiukwaji wa haki za binadamu na ni lazima ushughulikiwe, Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva,“tunaitaka serikali kufanya uchunguzi wa haraka kwa mtazamo wa kutenda haki na uwajibikaji ili kukomesha mzunguko wa ukwepaji sheria. Tumepeleka timu ikiwa na wachunguzi wa uhalifu pamoja na wapelelezi na watawafanyia mahojiano watu wa dini iliyoathirika ili kubaini nini kilitokea.”

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu  masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, limesema hali tete ya usalama imewatawanya maelfu ya watu huku 56,400 wakilazimika kuzihama nyumba zao na kuwa wakimbizi wa ndani Mopti. Tangu kutokea kwa shambulio Jumamosi iliyopita zaidi ya watu 2,000 wametawanywa tena wengi wakiwa ni watoto. Kwa sasa shule 523 kati ya shule 857 nchini humo zimefungwa huku eneo lililoathirika la Mopti idadi ya shule zilizofungwa ni mara mbili ya miaka miwili iliyopita na kuwaathiri watoto 150,000.