Watoto milioni 1 ni miongoni mwa wahanga wa kimbuga idai:UNICEF

23 Machi 2019

Katika taarifa iliyotolewa hii leo mjini Beira na Maputo Msumbiji, Geneva Uswisi  na New York Marekani, Henrietta Fore mkurugenze mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF amenukuliwa akisema,“tunakimbizana na muda ili kuwasaidia
na kuwalinda watoto katika maeneo yaliyoathirika nchini Msumbiji.”

 

Amesema hayo mwishoni mwa ziara yake mjini Beira, moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na kimbunga Idai.

Kwa mujibu wa makadirio ya awali ya serikali ya Msaumbiji, watu milioni 1.8 nchini kote, wakiwemo watoto 900,000 wameathiriwa na kimbunga kilichoipiga nchi hiyo wiki iliyopita. Hata hivyo maeneo mengi bado hayajafikiwa na UNICEF pamoja na wadau wake walioko nchini humo wanafahamu kuwa idadi ya mwisho ya waathirika itakuwa kubwa zaidi.

“Hali itakuwa mbaya kabla ya kutengamaa. Mashirika ya misaada hayajaweza kuanza kutathimini ukubwa wa uharibifu. Vijiji vizima vimesambaratishwa, majengo yamebomoka, shule na vituo vya afya vimeharibiwa. Wakati shughuli za utafutaji na uokoaji zinaendelea, ni muhimu kwamba tuchukue hatua zote muhimu kuzuia kuenea kwa magonjwa yanayosambazwa na maji, suala ambalo linaweza kubadili janga janga kubwa zaidi." Amesema Bi Fore.

UNICEF inasikitishwa mafuriko pamoja na hali ya mrundikano mkubwa wa watu katika makazi, hali duni ya usafi, maji yaliyotuama na vyanzo vya maji vilivyochafuliwa, vinawaweka watu katika hatari ya magonjwa kama vile kipindupindu, malaria na kuhara.

Tathimini ya awali mjini Beira inaonesha kuwa zaidi ya madarasa 2,600 yameharibiwa, pia vituo vya afya 39 viko katika hali mbaya. Takribani nyumba 11,000 zimebomolewa kabisa.

“Hali hii itakuwa na matokeo mabaya sana kwa elimu ya watoto, afya na ustawi wa kiakili” amesema Bi Fore.

Aidha Bi Fore ameongeza kusema kuwa watahitaji dola za kimarekani milioni 30 katika hatua ya kwanza ya kupambana na hali ilivyo huku wakitegemea wadau wengine kujitokeza kuwasaidia maelfu ya watoto na familia zinazohitaji msaada.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter