Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, yanaua kimya kimya Sudani Kusini-WHO.

Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs
WHO
Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs

Magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, yanaua kimya kimya Sudani Kusini-WHO.

Afya

Shirika la Afya duniani WHO limetahadharisha kuhusu magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika NTDs ambayo kwa mujibu wa shirika hilo yanawaathiri kimya kimya watu zaidi ya bilioni moja duniani kote  wengi wao wakiwa katika nchi za Afrika kama  Sudan Kusini. 

WHO imeyaorodhesha magonjwa 20 ya kitropiki yaliyosahaulika yaani NTDs ambayo yanawaathiri watu maskini, walioko hatarini  ai na wakiwa hawana uwezo wa kuyafikia maeneo mengine ya nchi hiyo changa barani Afrika..

 

Afisa wa WHO Dkt Evance Liyosi akihojiwa na redio Miraya ya ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini, anasema WHO kwa kushirikiana na wizara ya Afya ya Sudan Kusini wanachora ramani kuonesha eneo na ukubwa wa magonjwa haya ili waongeze juhudi za kuyakabili, “Hapa tuna magonjwa kama malale,  ugonjwa wa vikope unaoathiri macho,  kichocho, upofu na matende” 

Ameongeza kuwa Sudan Kusini ni moja ya nchi zilizoathirika zaidi barani Afrika ukiacha nchi kama vile Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Ethiopia.

Naye daktari Richard Lagu wa  Sudan Kusini akifafanua anasema magonjwa haya mengine yanaambukizwa na fangasi, mengine bakteria, virusi na mengine haijafahamika chanzo chake. 

Na akieleza sababu ya kwa nini yanasahaulika anasema ni kwa sababu  mengi  hayana athari zinazoonekana ndani ya muda mfupi kama ulivyo ugonjwa kama Malaria, nchi nyingi haziyapi kipaumbele magonjwa haya japokuwa ni ya hatari sana hasa kwa watu masikini , "Ukiangalia idadi ya watu wetu hii leo, asilimia 80 wako vijijini,  na pia kiwango cha umaskini kiko kwenye asilimia 52 hivi, na hawa ndiyo wameathirika zaidi. Sasa tumeweka sera na mikakati ya namna gani tunatoka kwenye kuyadhibiti haya magonjwa hadi kwenye kuyatokomeza  lakini bado hatuongelei kudhititi maana nchi nyingine zimeshavikia kwenye kutokomeza lakini tunaelekea huko."