Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la ushirikiano wa kusini-kusini lakubaliana mkakati wa kufikia ajenda 2030

Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa wakati ya kufunga pazia mkutano wa ngazi ya juu wa pili kuhusu ushirikiano wa kusini-kusini Buenos Aires, Argentina.
United Nations
Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa wakati ya kufunga pazia mkutano wa ngazi ya juu wa pili kuhusu ushirikiano wa kusini-kusini Buenos Aires, Argentina.

Kongamano la ushirikiano wa kusini-kusini lakubaliana mkakati wa kufikia ajenda 2030

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa ambao ni wa ngazi ya juu kuhusu ushirika wa Kusini-Kusini au BAPA+40 umekunja jamvi  leo Ijumaa katika mji mkuu wa Argentina Buenos Aires, kwa makubaliano ya nchi 160 wanachama kuhuisha upya dhamira ya kuchagiza na kuwekeza katika ushirikiano wa aina hiii baina ya nchi wanachama.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mkutano huo, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, Achim Steiner amesema. “kongamano limetoa ari inayohitajika kwa ajili ya kuweka njia ya ushrikiano wa kusini-kusini na ushirikiano wa kaskazini-kusini."

Bwana Steiner ameongeza kuwa kwa kutathmini mabadiliko yaliyotokea katika uchumi wa dunia, maendeleo, na uhai wa binadamu tangu kuanza kutiwa saini kwa BAPA miaka 40 iliyopita ni dhahiri kwamba hakuna ukomo kwa yale yanayoweza kupatikana kwa kufanya kazi pamoja.

Aidha ameongeza kuwa wameunda ushirikiano mpya kwa ajili ya juhudi za sasa na baadaye na kuona fursa zilizopo. Akitoa wito kwa nchi wanachama kuongeza hatua walizozipata kwa kipindi cha miaka 40 kwa ajili ya kutatua changamoto zinazokabili dunia wakati huu.

Ushirika wa Kusini-Kusini kama lilivyo jina lenyewe linamaanisha ushirikiano wa kiufundi miongoni mwa nchi zinazoendelea zilizoko eneo la Kusini mwa dunia . Pia ni nyenzo inayotumiwa na nchi, serikali, mashirika ya kimataifa , Wanazuoni, asasi za kiraia na sekta binafsi kushirikiana na kubadilishana ujuzi , uzoefu, ulelewa na miradi iliyofanikiwa katika baadhi ya maeneo kama vile maendeleo ya kilimo, haki za binadamu, ukuaji wa miji , afya, mabadiliko ya tabianchi na kadhalika.

Ushirika wa pande tatu kama lisemavyo jina lake unahusisha wadau watatu , wawili kutoka upande wa Kusini na mmoja kutoka Kaskazini. Inaweza kuwa ni shirika la kimataifa linatoa msaada wa kifedha kwa mataifa ya Kuisni kwa kubadilishana na msaada wa kiufundi wa kitu maalum au nada maalum.

Matokea ya mkutano yanatambua kwamba ushirikiano wa kusini-kusini na kaskazini-kusini unachangia katika utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu kwa ajili ya kutomkomeza umaskini katika aina zote kwani inabeba maono sawa ya maendeleo ikiwemo kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Halikadahlika inahimiza umuhimu wa ushirikiano wa kaskazini-kusini wakati upande wa tatu iwe ni nchi iliyoendelea au shirika linasaidi nchi za kusini-kusini na raslimali au ujuzi.

Tamko la kisiasa pia linatoa wito kuimarishwa kwa ushirikiano wa aina mbili na kunazingatia kwamba kumekuwa na mabadiliko ikilinganishwa na wakati ulianzishwa mwaka 1978.

Mfano wa ushirikiano wa nchi nyingi

Akihutubia kikao hicho cha kufunga kongamano hilo, rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa, amehimiza matokeo chanya ya ushirikiano wa nchi nyingi katika kuleta matokeo mazuri kufuatia ushirikiano. Bi Espinosa amesema, “juhudi zetu zimekuwa za kutia moyo kwani nyaraka ya mwisho inaonyesha mabadiliko katika ushirikiano wa kusini-kusini na inatoa mwelekeo wa baadaye. Inafungua fursa nyingi na kupanua wigo wa ushikamano katika ushirikiano hata na nchi zilizoendelea na wadau wengine. Ushirkiano wa kaskazini-kusini unawajumuisha wadau muhimu na fursa za ripoti za hiari ambazo zitatuwezesha kutathimini athari za ushirikiano."

Matokeo chanya

Bwana Steiner ameongeza kuwa, “miaka arobaini tangu kuzaliwa kwa wazo la ushirikiano wa kusini-kusini na kaskazini-kusini takriban nchi 150 wamerejea Buenos Aires sio tu kusherehekea miaka 40 ya wazo ambalo linaendelea kubadilika lakini pia kushiriki katika kuroa mwelekeo kwa ajili ya siku za usoni."

Mkuu huyi wa UNDP ametaja kwamba jamii ya kimataifa hususan nchi zilizoko kusini zinatarajia dunia kushirikiana kwa ajili ya kutekeleza mkataba wa Paris na kulinda bayoanuai akisema, “nyingi ya fursa zilizopo sasa zinaedndelezwa katika mataifa ya kusini na pengine yanatoa matumaini ya kubadili maendeleo ya kiuchumi katika kitu tofauti kando na hali ya kuchimba au kuchafua mazingira."

Kwa upande wake mkurugenzi wa ofisi ya Umoja wa mataifa ya ushirika wa Kusini-kusini Jorge Chediek, amesema makubaliano ya pamoja yanaleta nchi pamoja katika kudhamiria kushirikiana zaidi kuhusu maswala ya kimataifa.  

Aidha bwana Chadiek amesema, hatua muhimu imefikiwa katika kutambua ushirikiano wa kusini-kusini na kasakzini-kusini kama kiungo muhimu katika ushirikiano wa kimataifa. Akiongeza, “kulikuwa na migawanyiko lakini makubaliano yanahakikisha kwamba ni kiini na muhimu."

Mkutano huu uliwaleta pamoja nchi wanachama 160 na zaidi ya washiriki 4000 kutoka mashirika ya yasiyo ya kiserikali, ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia katika ziku nne za BAPA+40.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa yanatoa wito kwa katibu Mkuu kutoa ripoti kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayoa ambayo ni muhimu katika kufikia ajenda yam waka 2030 na malengo yake 17 ya maendeleo endelevu, SDGs.