Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yasaidia matibabu kwa zaidi ya waathirika 10,000 wa kimbunga Idai msumbiji

Ni tarehe 21 Macji 2019 familia ikiwa imesimama mbele ya makazi yao ya muda ambayo wameyajenga Beira Msumbiji baada ya kimbunga Idai kuyasambaratisha makazi yao.
UNICEF
Ni tarehe 21 Macji 2019 familia ikiwa imesimama mbele ya makazi yao ya muda ambayo wameyajenga Beira Msumbiji baada ya kimbunga Idai kuyasambaratisha makazi yao.

UN yasaidia matibabu kwa zaidi ya waathirika 10,000 wa kimbunga Idai msumbiji

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la afya ulimwenguni WHO limepeleka wahudumu wa afya na vifaa kwenye vituo takribani 53 vilivyoathirika vibaya na mafuriko nchini Msumbiji huku mkurugenzi mtendaji akizuru maeneo yaliyoathirika kukusanya na kuchagiza msaada kwa ajili ya watoto na familia zao.

Kuendelea kuchukua hatua za kusaidia wahanga wa kimbunga Idai nchini Msumbiji WHO imepeleka timu ya wataalam wa kudhibiti majanga na huduma za dharura, dawa na vifaa vingine.

Shirika hilo linasema lengo ni kukidhi mahitaji ya msingi ya huduma za za kiafya kwa watu 10,000 kwa muda wa miezi mitatu mbali ya kutibu majeruhi wanaoendelea kujitokeza kutokana na kuendelea kwa hali mbaya ya hewa.

Umoja wa Mataifa wasikitishwa na Idai

Kufuatia ukubwa wa zahma hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na idadi kubwa ya vifo na kughubikwa na majonzi akishuhudia picha za madhila yanayowakumba watu waliokumbwa na kimbunga Idai mjini Beira Msumbiji tangu usiku wa Machi 14 na kisha kupanua wigo hadi Malawi na Zimbabwe na kusababisha janga kubwa la kibinadamu.

Hata hivyo amesema ametiwa moyo na kusifu juhudi za kitaifa na kimataifa za kuendelea kuwasaka manusura kwa kufanya kazi usiku na mchana kuokoa maisha ya maelfu ya wengine na pia kwa kusambaza misaada inayohitajika kwa manusura ambao wengi wamepoteza kila kitu. Guterres ameongeza kuwa mashujaa hawa sio tu wameokoa watu kutoka katika paa za nyumba bali pia wamefikisha msaada wa chakula, tembe za kusafisha maji na misaada mwingine ya kibinadamu inayohitajika. Ameongeza kuwa hivi sasa mazao yote yakiwa yamesambaratishwa nchini Msumbiji , watu wengi wako katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula  katika nchi zote tatu  huku nyumba, shule, hospital na barabara zikiwa zimesambaratishwa. Ametoa wito na ombi kwa jumuiya ya kimataifa kushikamana na watu wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe akisema kinachohitajika sasa ni fedha ili kukabiliana na athari katika siku, wiki na miezi mingi ijayo.

Waliopoteza maisha na waliotawanywa

Serikali ya Msumbiji tayari imethibitisha vifo 280 vilivyosababishwa na janga hili na watu wengine zaidi ya 660,000 wametawanywa katika jimbo la kati la Sofala eneo lililoathirika zaidi na kimbunga. Maelfu ya watu wa Msumbiji wanakosa huduma za malazi, maji safi, chakula na umeme.

Changamoto za kuwafikia waathirika

Hadi sasa barabara nyingi hazipitiki kutokana na mafuriko pia kuna upungufu mkubwa wa mafuta kwa ajili ya helkopta za misaada ambazo ndio njia pekee ya kufika maeneo yasiyofikika. Kwa mujibu wa WHO vituo vya afya 53 vimesambaratika na kiwango kamili cha uharibufu bado hakijafahamika sababu kuna maeneo mengine ambayo hayajafikiwa. Wataalam wa WHO kwa hivi sasa wanasaidia katika masuala ya kiufundi, mipango, mawasiliano na juhudi za kuzuia magonjwa kama kipindupindu na malaria. Lakini pia WHO inaisaidia serikali kutathimini na kusaili msaada wa dharura wa madaktari kutoka katika nchi mbalimbali.

Mshikamano

Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Henrietta Fore anazuru maeneo yaliyiathirika na kimbunga Idai kwenye jimbo la Beira na atakuwa huko hadi Jumamosi wiki hii lengo likiwa ni kushuhudia hali halisi ya athari za kimbunga hicho kwa Watoto na familia zao na kusaidia katika misaada ya kibinadamu.

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Msataifa la uhamiaji IOM limetoa ombi la kikanda ili kukusanya msaada kutoka jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya waathirika katika nchi zote tatu Msumbiji , Malawi na Zimbabwe. Zaidi ya maiti 120 zilisombwa na maji kutoka Zimbabwe hadi Msumbiji ambako zimezikwa na wakazi wa eneo zilizkookotwa. Na Malawi madaraja manne muhimu yamesambaratishwa na kimbunga hicho.