Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanoishi katika mizozo wana hatari ya kufa na magonjwa yatokanayo na maji mara tatu zaidi-UNICEF

Katika makazi ya muda Ain Issa kilometa 50 kaskazini mwa Raqqa nchini Syria, Horriya mwenye umri wa miaka 12 abeba mtungi wa maji.(2017)
UNICEF/Souleiman
Katika makazi ya muda Ain Issa kilometa 50 kaskazini mwa Raqqa nchini Syria, Horriya mwenye umri wa miaka 12 abeba mtungi wa maji.(2017)

Watoto wanoishi katika mizozo wana hatari ya kufa na magonjwa yatokanayo na maji mara tatu zaidi-UNICEF

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 wanaoishi katika nchi zilizoathiriwa na mizozo kwa wastani wako hatarini mara tatu zaidi kufa kutokana na magonjwa ya kuharisha yanayosababishwa na ukosefu wa maji salama, huduma ya kujisafi na usafi kuliko matokeo ya ukatili kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maswala ya watoto, UNICEF.

Ripoti hiyo iliyopewa jina, “maji chini ya moto/Maji motoni?” inaangazia vifo vya watoto katika nchi 16 zinazoshuhudia mizozo ya muda mrefuambako tathmini zinaonyesha kwamba katika mizozo mingi, watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wako katika hatari mara 20 zaidi kufa kutokana na magonjwa ya kuharisha yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama na huduma za kujisafi kuliko visa vya ukatili.

Ripoti ya UNICEF imemnukuu mkurugenzi mkuu wake, Henrietta Fore akisema, “uwezekano huo tayari unawakabili watoto walio katika maeneo ambako kunashuhudiwa mizozo ya muda mrefu, wengi wakishindwa kufika sehemu za maji salama, ukweli ni kwamba kuna watoto wengi zaidi wanoafariki kutokana na kutopata maji salama kuliko risasi.”

UNICEF imesema bila maji salama na huduma za kujisafi watoto wako hatarini kupata utapiamlo na magonjwa yanayoweza kuzuilika ikiwemo,kuhara, homa ya matumbo, kipindupindu na polio. Halikadhalika ripoti imesema wasichana wako katika hatari ya ukatili wa kingono wakati wakisaka maji au matumizi ya huduma ya vyoo huku wakikabiliwa na hali ngumu hususan wakati wa hedhi ambapo hukosa kuhuduhuria shule iwapo shule hazina huudama za maji na kujisafi.

Kwa mujibu wa ripoti, hali inakuwa mbaya zaidi pale minudombinu inalengwa, watoa misaada wanashambuliwa na kukatizwa kwa huduma zaumeme ambazo zinaendesha mifumo ya maji na huduma ya kujisafi. Aidha mizozo ikiathiri ufikiaji na uwezekano wa kukarabati mifumo hiyo pale inapohabribika

Bi Fore amesema, “mashambulizi ya kulenga ya mifumo ya maji na huduma za kujisafi ni mashambulizi dhidi ya watoto, maji ni haki ya msingi na ni huduma muhimu katika maisha".

Kwa mantiki hiyo UNICEF imetoa wito kwa serikali na wadau kusitisha mashambulizi dhidi ya mifumo ya maji na huduma za kujisafi, kuoanisha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu na uimarishaji wa mifumo endelevu ya maji na huduma za kujisafi kwa wote, kuwezesha serikali na mashirika ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kutoa huduma za maji na kujisfai wakati wa dharura.