Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya kupata maji na vifaa vya kujisafi ni chachu ya kutomwacha yeyote nyuma-Mtaalam UN

Wakimbizi wa ndani jimbo la Darfur Sudan wanakabiliwa na changamoto nyingi na ugumu wa kupata maji safi. Pichani ni msichana na kaka yake wakiwa katika kituo cha maji safi cha Abu-Shok kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani illi kuteka maji
UNAMID/Mohamad Mahady
Wakimbizi wa ndani jimbo la Darfur Sudan wanakabiliwa na changamoto nyingi na ugumu wa kupata maji safi. Pichani ni msichana na kaka yake wakiwa katika kituo cha maji safi cha Abu-Shok kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani illi kuteka maji

Haki ya kupata maji na vifaa vya kujisafi ni chachu ya kutomwacha yeyote nyuma-Mtaalam UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Haki ya binadmau ya kupata maji salama na huduma ya kujisafi kwa wote ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, lakini pia ni ufunguo wa kufurahia haki zingine za bindamu amesema mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kupata maji salama na huduma za kujisafi, Léo Heller katika kuelekea siku ya maji duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Machi 22.

Bwana Heller amesema wanalenga kuhakikisha   kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma katika kufikia huduma za maji na kujisafi na ili nchi zifikie haki za binadamu ni lazima kutimiza mahitaji ya walio hatarini zaidi, na kubadili mawazo ya kijadi ya kutoa huduma kwanza kwa wale wanaoweza kugharamia.

Mtaalam maalum huyo amesisitiza kwamba utaratibu unaozingatia haki za binadamu unaweza kutoa mwelekeo dhabiti kwani unaleta sura ya kibinadamu na kutoa muongozo kwa serikali kwa ajili ya kupanga sera zao kulenga watu walioko hatarini na kutoa fursa ya kukabiliana na vitu vinavyoweza kusababisha ukiukwaji wa haki hizo.

Bwana Heller ameongeza kuwa maji na huduma za kujisafi zina uhusiano na mambo mengi katika maisha yetu ikiwemo, afya, chakula, elimu, umasikini na usalama wa kimwili. Hata hivyo, mtu mmoja kati ya watatu kote ulimwenguni hana huduma ya maji safi na vifaa vya kujisafi na zaidi ya nusu ya watu kote ulimwenguni hawapati huduma za kujisafi.

Mtaalam maalum hyo amesema juhudi mujarabu za mataifa za kupata suluhu ya changamoto hizo zinaweza kusongeshwa mbele iwapo watu waliohatarini zaidi au wanaohitaji msaada zaidi watashrikishwa.