Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na serikali wachunguza madai ya kutiwa sumu katika chakula cha WFP Uganda.

Mgao wa chakula wa WFP kwa wahusika.
WFP/Photolibrary
Mgao wa chakula wa WFP kwa wahusika.

WFP na serikali wachunguza madai ya kutiwa sumu katika chakula cha WFP Uganda.

Afya

Shirika la Mpango wa chakula duniani (WFP) linashirikiana na serikali ya Uganda kuchunguza kilichosababisha kuugua kwa watu zaidi ya 282 baada ya kupokea msaada wa chakula aina ya nafaka kutoka kwa WFP.

Kulingana na taarifa ya pamoja ya  WFP na serikali ya Uganda, uchunguzi wa pamoja umeanza na tayari kuna wataalamu kutoka pande zote walioko katika maeneo yalioathirika ili kubaini iwapo kuna uhusiano kati ya magonjwa yalioripotiwa na chakula kilichogawiwa na WFP katika juhudi zake za kushughulikia tatizo la  utapiamlo katika eno la Karamoja nchini humu .

Tarehe 12 mwezi huu, wizara ya afya ilipokea ripoti ya kuhusu uwezekano wa chakula hicho kutiwa sumu na mara moja walianzisha uchunguzi.

Tangu siku hiyo watu 262 wamelazwa hospitali wakiwa na dalili za kuchanganyikiwa kiakili, kutapika, maumivu ya kichwa, homa kali na maumivu ya tumbo.

Hata hivyo kati ya waathirika, watu 252 tayari wameruhusiwa kutoka vituo vya afya mbalimbali hospitalini baada ya kupata matibabu.

Hamna visa vipya ambavyo vimeripotiwa tangu jana tarehe 18 Machi.

Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kwamba kuna watu  watatu ambao walifariki dunia, moja kwenye hospitali ya Matany wilayani Napak na wengine wawili walifariki dunia wakiwa majumbani kwao.

Sampuli za damu na mkojo za wathirika vinachunguzwa katika maabara ya serikali.  Sampuli za chakula pia zimepelekwa kwenye kampuni ya Intertek Kenya LTD kule Mombasa Kenya na zingine Johannesburg katika kituo cha huduma ya uchunguzi cha Intertek Testing Services S.A. LTD nchini Africa Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Ijumaa ya tarehe 15 Machi, WFP kwa kushirikiana na serikali waliamuru kusitishwa mara moja ugawaji wa nafaka katika eneo la Karamoja na katika wilaya zinazohifadhi wakimbizi ambako nafaka hizo zilikuwa zinagawiwa wakisema hizo ni hatua za tahadhari hadi pale uchunguzi utakapokamilika 

Waziri wa masauala ya Karamoja John Byabagambi, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za afya, Dr. Henry Mwebesa, Mkurugenzi wa WFP, Khidir Daloum, mafisa wa ubora wa bidhaa nchini Uganda wlaitembelea wathirika hapo Jumatau tarehe 18 Machi.