Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu ya maandamano ya Gaza ikijongea, UN yaitaka Israel kujirekebisha.

Tume ya uchunguzi wa maandamano ya 2018 kwenye eneo linalokaliwa la Palestina wakizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis 28 Februari 2019. Betty Murungi ni mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Santiago Cantoni (Katikati) mwenye kiti wa tume na Sara
PICHA na UN/Violaine Martin
Tume ya uchunguzi wa maandamano ya 2018 kwenye eneo linalokaliwa la Palestina wakizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis 28 Februari 2019. Betty Murungi ni mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Santiago Cantoni (Katikati) mwenye kiti wa tume na Sara

Kumbukumbu ya maandamano ya Gaza ikijongea, UN yaitaka Israel kujirekebisha.

Amani na Usalama

Tume huru ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuhusu maandamano katika eneo linalokaliwa la Palestina, hii leo mjini Geneva Uswisi, mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, imewasilisha matokeo ya uchunguzi wake baada ya kuchunguza mauaji na majeruhi yaliyotokea kwenye uzio unaotenganisha Israel na Gaza wakati wa maandamano yaliyofanyika mwaka jana.

Ripoti ya tume hiyo imechunguza maelekezo ya vikosi vya ulinzi vya Israel kwa walenga shabaha kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wa kipalestina.

Mwenyekiti wa tume, Santiago Canton kutoka Argentina, ameliambia Baraza la Haki za Binadamu,  “tunawasilisha ripoti hii ya kina ikiwa na ombi la dharura kwa Israeli kuhakikisha mara moja kwamba sheria za ushiriki wa vikosi vyao vya usalama zimerekebishwa ili kuzingatia viwango vya kimataifa vya kisheria. Maadhimisho ya mwaka mmoja wa maandamano Gaza yanakuja  chini ya wiki mbili zijazo. Tunasikia kwamba kutakuwa na umati mkubwa katika maeneo ya maandamano rasmi. Matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyotokea tarehe 30 Machi, 14 Mei na 12 Oktoba 2018 hayapaswi kujirudia.”

Tume imebaini kuwa vikosi vya usalama vya Israel viliwapiga risasi na kuwajeruhi waandamanaji 6016 kwa kutumia risasi za moto. Watu 189 kati yao walipoteza maisha katika eneo la maandamano, 183 kati yao wakiwa wamekufa kutokana na kupigwa risasi za moto.

“Tunapinga vikali kusema kuwa kilichofanyika kina vigezo vyote vya haki za binadamu. Kwa tukio hili la watu 4903 wasio na silaha kupigwa risasi miguuni tena wakiwa wamesimama mbali na warusha risasi” ameongeza Bwana Canton.

Naye Kamishina Kaari Betty Murungi wa Kenya amesema, “tume inazo sababu nzuri za kuamini kwamba wakati wa maandamano, askari wa Israeli waliwaua na kuwajeruhiwa raia ambao hawakuwa wanahusika moja kwa moja katika mvutano au kutoa tishio la karibu kwa Jeshi la Usalama wa Israeli, au hata kwa raia wa Israel. Vikosi vya Usalama vya Israeli vilifanya ukiukwaji wa haki za kimataifa za kibinadamu na sheria za kibinadamu. Baadhi ya ukiukwaji huo unaweza kusababisha uhalifu wa vita au uhalifu dhidi ya ubinadamu, na lazima mara moja Israel ifanye uchunguzi.”