Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania na mbinu bunifu za kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi  ya Mkapa, Hellen Mkondya Senkoro akihojiwa na Arnold Kayanda wa UN News kando mwa mkutano wa CSW63.
UN News/Patrick Newman
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Hellen Mkondya Senkoro akihojiwa na Arnold Kayanda wa UN News kando mwa mkutano wa CSW63.

Tanzania na mbinu bunifu za kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto

Wanawake

Ni mkutano ambao umewaleta pamoja takribani washiriki 9000 kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kuanzia nchi za kipato cha juu, kati na cha chini ili kila mmoja apate kujifunza kutoka kwa mwingine. Na katika tukio lililoandaliwa na Tanzania kandoni mwa mkutano huo ndipo Dkt Ellen Mkondya Senkoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Benjamin Mkapa na Wakili Haika Harrison Ngowi wa shirika la Save the Children katika mahojiano haya na Arnold Kayanda wameieleza UN News Kiswahili kile ambacho wamekuja kubadilishana na wenzao wa mataifa mengine. 

Dkt Ellen anasema wameibuka na mbinu bunifu za kuboresha afya zikiwemo kuhakikisha kuna wahudumu wa afya wa kutosha.

Akifafanua amesema, “tumeweza kuajiri zaidi ya watumishi 1500 ambao wana kada mbalimbali, kuna madaktari, wauguzi na wafamasia ambao wameenda kufanya kazi maeneo ya vijijini na wamefika katika hospitali za mikoa na tumefikia zaidi ya aslimia 50 ya vituo vya afya. Na tunakubaliana na serikali kwamba wanapomaliza miakataba kuisha basi wataingia kwenye mikataba ya kudumu ya serikali. Lakini la pili ili kupunguza umbali kwa akina mama wanaojifungua, hasa wale wanaojifungua kwa upasuaji tuliona tuimarishe vituo vya afya katika kuhakikisha wanapata maeneo ya kufanyia upasuaji kwa hivyo inaleta uhakika kwa mama na mtoto.”

Haika Harrison Ngowi wa Save The Children Tanzania akihojiwa na UN News wakati wa CSW63
UN/Patrick Newman
Haika Harrison Ngowi wa Save The Children Tanzania akihojiwa na UN News wakati wa CSW63

Kwa upande wake Wakili Haika kutoka Save the Children anaeleza shirika lao linasaidiana na serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na visiwani.

Amesema, “kwa Zanzibar, Save the Children imesaidia kuanzisha vituo sita vya huduma kwa pamoja yaani huduma za mkono kwa mkono ambapo wadau wote wanakuwa kwenye kituo kimoja, kwa mfano polisi, mtu wa saikolojia, ustawi wa jamii wote wawepo pale ili mtoto ambaye ameshaumizwa asihangaike kupata hizi huduma. Kwa Dar es Salaam ipo pale Mnazi mmoja na kwa Shinyanga iko Shinyanga mjini, Shinyanga vijijini na Kahama. Pia tunashirikiana na Serikali kuona tunavyoweza kuanzisha nyingi zaidi.”