Shehena ya kwanza ya chakula yawasili Hodeidah tangu Mei 2018-WFP

Baada ya miezi ya ushawishi na kubembeleza , meli ya MV Elena imekamilisha kupakua shehena ya msaada wa kibinadamu kwenye bandari ya Hodeidah ikiwa ni meli ya kwanza iliyoshoheni msaada wa shirika la mpoango wa chakula duniani WFP kuwasili bandari hiyo tangu Mei 2018.
Akifafanua kuhusu hilo msemaji wa WFP Herve Verhoosel amesema kutowasili kwa kontena zozote tangu Mei mwaka jana kwenye bandari ya Hodeidah inamaanisha kwamba "makontena yote ya chakula cha msaada yamekuwa yakipelekwa bandari ya Aden, ambayo ni ndogo na haraka ikawa na msongamano. Na kupunguza msongamano huo ikaanza kutumia bandari ya Salalah iliyoko Omani kusafirisha mizigo lakini ngano na nafaka zimeendelea kuwasili hodeidah katika mezi michache iliyopita.”
Shehena hiyo ya kwanza ya WFP ilikuwa na makontena 440 yaliyofungasha mafuta ya kupikia yakihamishwa kutoka bandari ya Salalah Oman. Na meli hiyo imerejea Salalah kwa raundi ya pili ili kufungasha makontena mengine 481yaliyofungasha tani zaidi ya 8300 za mafuta ya kupikia zilizowasili wiki iliyopita.
Baada ya safari hii WFP inasema meli hiyo inatarajiwa kuanza safari mpya kuleta makontena Zaidi ya misaada ya kibinadamu kwenye bandari ya Hodeidah kutokea katika bandari zingine.
WFP imekaribisha hatua hiyo kwamba sasa makontena yaliyosheheni misaada ya kibinadamu yanaweza kuwasili tena mjini Hodeidah, kwani kama inavyofahamika Hodeidah ni barandari muhimu nchini yemen kwani asilimia 90 ya chakula kinaingizwa kutoka nje na asilimia 70 ya safari zake zinapitia bandari ya Hodeidah.