Pamoja na maambukizi mapya ya VVU kupungua duniani, bado hali ni tete kwa wanaojidunga dawa za kulevya-UNAIDS.

13 Machi 2019

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na UKIMWI, UNAIDS iliyozinduliwa leo mjini Geneva Uswisi inaonesha pamoja na kupungua kwa maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI, VVU, duniani kote, bado maambukizi miongoni mwa wanaotumia sindano kujidunga madawa ya kulevya hayapungui.

Ripoti pia inaonesha kuwa asilimia 99 ya watu wanaojidunga dawa za kulevya  wanaishi katika nchi ambazo hazitoi huduma ya kupunguza madhara.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé anasema, “UNAIDS inasikitishwa na maendeleo madogo kwa wanaotumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano, kwasababu ya kushindwa kwa nchi nyingi kutekeleza kwa kutumia mbinu zinazoendana na msingi wa haki za binadamu katika masuala ya matumizi ya madawa ya kulevya. Kwa kuwaweka watu katika kituo na kuhakikisha wanapata huduma ya afya na za kijamii kwa utu na bila kubaguliwa au kuwafanya kuwa ni waliofanya makosa, maisha yanaweza kuokolewa na maambukizi mapya ya VVU kupungua.”

Ripoti hii mpya ya UNAIDS, yenye jina afya, ‘haki na madawa: kupunguza madhara, kutokomeza ubaguzi dhidi ya watu wanaotumia madawa ya kulevya’, inaonesha kuwa katika watu milioni 10.4 wanaojidunga madawa kulevya kwa kutumia sindano, kwa mwaka 2016, zaidi ya nusu yao walikuwa wanaishi na homa ya ini (hebatitis C) na mmoja kati ya 8 alikuwa anaishi na VVU.

Hali hiyo inaonesha kuwa kukiwa na huduma za kupunguza madhara kama vile kuwapatia sindano, matibabu ya utegemezi wa dawa, kuwapima VVU na kuwapatia matibabu kunaweza kusongesha hatua katika kuzuia maambukizi mapya miongoni mwa wajidunga.

Hata hivyo, ni nchi chache wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo zimetekeleza makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2016 katika moja ya vikao maalumu katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu tatizo la madawa ya kulevya duniani ili kuanzisha hatua mathubuti za afya ya jamii ili kuboresha matokeo ya afya kwa watu wanaotumia madawa ya kulevya.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter