Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya watoto jimboni Kasai DRC ni ya kutisha-UNICEF

Hali ya watoto nchini DRC imeendekea kuathiriwa na vita isiyokoma.
UNICEF/Kate Holt
Hali ya watoto nchini DRC imeendekea kuathiriwa na vita isiyokoma.

Hali ya watoto jimboni Kasai DRC ni ya kutisha-UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linakadiria kuwa watoto 260,000 kwenye eneo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi. Flora Nducha na maelezo kamili.

UNICEF inasema watoto hao wanahitaji huduma za kuokoa maisha yao kwa kuwa unyafuzi unatishia maisha yao ikisema idadi inajumuisha pia watoto wengine waliokimbilia eneo hilo la Kasai na familia zao wakitokea majimbo ya jirani ya Kwilu na Kwango.

Mmoja wa wazazi wa watoto hao amesema mtoto wake alianza kula mchanga kwa sababu ya njaa kali ilhali mzazi mwingine amesema mtoto wake mwenye umri wa miaka minne alikabiliwa na njaa kali wakati wakikimbia kutoka msituni.

UNICEF inasema ukosefu wa usalama kwenye eneo la Kasai kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2018 umesababisha idadi kubwa ya watu kukimbia makazi yao, haki za watoto zikipuuzwa na utapiamlo uliokithiri miongoni mwa watoto.

Hata hivyo hali ya usalama imeripotiwa kuwa shwari katika baadhi ya maeneo lakini bado kiwango cha utapiamlo ni cha juu.

Madeleine Kabondia ni afisa afya, “Kituo cha afya kinatibu homa iwapo inahitajika na pia tunagawa chakula chenye lishe kwa watoto wenye utapiamlo.,”

Kwa mujibu wa UNICEF, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, imeshirikiana na wadau wake kutibu watoto 200,000 waliokuwa na unyafuzi huko Kasai.

Kurejea nyumbani kwa wakimbizi 300,000 wa DRC kutoka Angola kumeongeza shinikizo kwenye huduma za msingi jimboni Kasai ikiwemo huduma za afya.