Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maafisa wenye mamlaka wamehusika na ukiukwaji wa haki Sudan Kusini - Ripoti

Matatizo ya muda mrefu yamesababisha mateso makubwa kwa watu wa Sudan Kusini hasa  wanawake.
UN Photo/Isaac Billy
Matatizo ya muda mrefu yamesababisha mateso makubwa kwa watu wa Sudan Kusini hasa wanawake.

Maafisa wenye mamlaka wamehusika na ukiukwaji wa haki Sudan Kusini - Ripoti

Haki za binadamu

Ripoti ya tume ya  Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini  iliyowasilishwa leo mijini Geneva Uswisi, imebaini kuwa watu 23 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita waliokuwa katika ngazi ya mamlaka nchini humo, wanakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji  mkubwa wa haki za binadamu chini ya sheria za kimataifa kwa kutekeleza uhalifu mkubwa unaohusiana na vita nchini Sudan kusini.

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya Baraza Kuu la haki za binadamu, Yasmin Sooka  ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo Sudan kusini amesema , watuhumiwa hao na wengine waliotajwa hapoi awali wanaweza kukabiliwa na mkono wa haki mahakamani popote duniani  sio tu Sudan Kusini .Tume ililenga matukio yaliyotokea kati ya Mei na Juni 2018 katika Jimbo la Unity, magaribini mwa  Bahr el Ghazal, na huko Equatoria, yakiwemo unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji wa kikatili, utumwa wa ngono , utekaji nyara, ndoa za shuruti, mimba za kulazimishwa, na mauaji yaliyotekelezwa na vikosi vya serikali na pia wanamgambo wa upinzani.

Pia tume ilibaini kuwa  taarifa za UNICEF kwamba  zaidi ya asilimia 25 ya kesi zote zilizoripotiwa za unyanyasaji wa kijinsia zinazohusiana na migogoro, waathirika  wakubwa walikuwa ni watoto.

Wawakilishi hao wamesema mkataba wa amani uliotiwa saini hivi karibuni Sudan Kusini bado haujazaa matunda  kwa raia nchini humo kwasababu migogoro inayoendelea imesbabihsa  asilimia 60 ya idadi ya watu kukabiliwa na matatizo ya kutokuwa na uhakika  wa  chakula, na kwamba bado kuna wakimbizi milioni 2.2 ambapo milioni 1.9 kati yao ni wakimbizi wa ndani .

Ripoti imebaini pia kuwa, Sudan Kusini inabaki kuwa sehemu hatari zaidi duniani kwa wafanyakazi wa  mashirika ya kibinadamu kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Na  imetoa wito kwa Serikali ya Sudani Kusini kuchukua hatua za haraka kuelekea kuanzishwa kwa tume ya upatanisho na maridhiano, na  pia mamlaka ya fidia na kwamba Serikali ya Sudan Kusini na Umoja wa Afrika kwa pamoja waanzishe Mahakama ya pamoja nchini Sudan Kusini  ili kuchapuza mchakato wa kushughulikia kesi za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.