Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yahitaji fedha zaidi kusaidia wakimbizi wa ndani Burkina Faso

Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho nchini Burkina Faso(Machi 2019). Ukosefu wa usalama, mzozo wa chakula na mafuriko ni miongoni mwa vichocheo vya mzozo wa kibinadamu nchini humo.
OCHA
Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi ya Barsalogho nchini Burkina Faso(Machi 2019). Ukosefu wa usalama, mzozo wa chakula na mafuriko ni miongoni mwa vichocheo vya mzozo wa kibinadamu nchini humo.

UNHCR yahitaji fedha zaidi kusaidia wakimbizi wa ndani Burkina Faso

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linahitaji fedha za nyongeza kwa ajili ya kufanikisha operesheni zake za kusaidia wakimbizi wa ndani nchini Burkina Faso wakati huu ambapo dola milioni 27.3 zilizoombwa kwa ajili ya operesheni za mwaka 2018 zimefadhiliwa kwa asilimia 26 pekee.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Babar Baloch amewaambia waandishi wa habari kuwa wakimbizi hao wanatokana na kuendelea kwa hali ya kukosekana kwa usalama kaskazini mwa Burkina Faso.

Amesema ukosefu wa usalama umesababisha zaidi ya watu 115,000 kusalia wakimbizi  wa ndani huko wengine 11,000 wakilazimika kukimbia nchi hiyo na kusaka hifadhi nchi jirani.

“Ghasia pia zimekwamisha  watoa  huduma za misaada ya kibinadamu kufikia wakimbizi wa ndani nchini humo,” amesema Bwana Baloch akiongeza kuwa kutokana na hali hiyo, UNHCR ina  wasiwasi mkubwa na hali ya usalama kaskazini mwa nchi hiyo.

Amesema licha ya hatua zilizochukuliwa za kuimarisha usalama ikiwemo kupeleka vikosi vya kijeshi, baadhi ya maeneo ya Burkina Faso yameshuhudia ongezeko la ghasia, ghasia hizo zikilenga wahudumu wa kibinadamu na kukwamisha operesheni za kibinadamu kusambaza misaada.

Tangu mwaka 2015, Burkina Faso imekuwa ikishuhudia ongezeko la ghasia zikienda sambamba na matukio ya mashambulizi kwenye mji mkuu Ouagadougou pamoja na mashambulizi kwenye maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo.

Hofu zaidi ya UNHCR ni kwamba raia zaidi wanaweza kuathiriwa na ghasia hizo na kwa mantiki hiyo shirika hilo linaungana na wadau wengine wa kibinadmau kuomba hatua zaidi za usalama kwa raia na kuheshimiwa kwa wahudumu wa misaada ya kibinadamu ili misaada iweze kuendelea kusambazwa kwa wahitaji.

Zaidi ya asilimia 90 ya wakimbizi wa ndani nchini Burkina Faso wanaishi na jamii za wenyeji ambapo asilimia 70 wako ukanda wa Sahel ilhali asilimia 30 wako eneo la Djibo.