Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi Mkuu wa WHO azuru kituo cha Ebola kilichoshambuliwa hii leo DRC.

Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO azuru kituo cha Ebola kilichoshambuliwa hii leo DRC.

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus hii leo amekitembelea kituo cha matibabu ya Ebola katika eneo la Butembo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Kituo hicho cha Ebola ndicho wiki iliyopita kilishambuliwa na makundi ya watu wenye silaha. Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Butembo imeeleza kuwa kituo hicho kimeshambuliwa tena mapema leo.

Dkt Tedros amezungumza na wafanyakazi wa kituo hicho na akawashukuru kwa kujitolea kwao.

Ziara hii katika kituo cha Ebola cha Butembo inakuja wakati Dkt Tedros akikamilisha ziara yake ya siku tatu nchini DR Congo akiambatana na viongozi kutoka serikali ya Marekani na wa WHO. Viongozi hao pia katika siku hizi za ziara wamekutana na Rais wa DRC, viongozi wa serikali, mashirika na wananchi wengine ambao wameshiriki kwa namna mbalimbali katika mapambano dhidi ya Ebola. Dkt Tedros amesema, “Inaumiza moyo wangu kufikiria watoa huduma ya afya ambao wamejeruhiwa na afisa wa polisi ambaye amefariki hii leo kutokana na uvamizi katika kipindi ambacho tunawaomboleza wengine ambao walikufa katika uvamizi uliopita wakiwa katika shughuli ya kuilinda haki ya afya. Lakini hatuna chaguo isipokuwa kuendelea kuwahudumia watu wa hapa ambao ni kati ya waliko hatarini duniani.”

Dkt Tedros ameongeza kusema kuwa mashambulizi haya hayafanywi na jamii bali yanafanywa dhidi ya jamii na kuna wanaofaidika na hali hiyo kwa faida yao wenyewe.

“Watu wa Katwa na Butembo kama ilivyo katika jamii nyingine ambazo zimeaathiriwa na Ebola, wanataka na wanastahili mahali pa kuapata uangalizi na nafasi ya kuokolewa. Hawastahili kuteseka katika nyumba zao huku wakiwaambukiza wapendwa wao, hawastahili kuteseka katika vitu duni vya afya huku wakiwaambukiza wataalamu wa afya” Dkt Tedros amesisitiza.