Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu ni msingi wa maendeleo endelevu-Naibu Katibu Mkuu UN.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed  akihutubia mkutano wa 40 wa Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia mkutano wa 40 wa Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi.

Haki za binadamu ni msingi wa maendeleo endelevu-Naibu Katibu Mkuu UN.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed hii leo akihutubia mkutano wa 40 wa Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi amesisitiza juu ya uhusiano wa karibu uliopo kati ya haki za binadamu na maendeleo endelevu, “Ninataka kusisitiza dhamira yetu ya kutoa haki na ustawi wa watu kupitia kutekeleza Malengo ya maendeleo endelevu. Haki za binadamu ni sehemu muhimu katika maendeleo endelevu na maendeleo endelevu ni chombo muhimu katika utambuzi wa haki zote za binadamu.”

Aidha amesisitiza kuwa kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu au SDGs inamaanisha kutambua hali ya kutegemeana na kutotengana kwa haki zote za kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kiraia na kisiasa, pamoja na haki ya maendeleo. Na inamaanisha kutoa haki hizi hatua kwa hatua.

Bi Mohammed pia amewaambia wajumbe wa mkutano kuwa kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu inamaanisha kuwa watu wanaweza kufikia haki zao za makazi bora, maji safi, huduma ya afya, elimu na chakula pia haki yao ya kushirikia katika maamuzi kuhusu maisha,“na kimsingi kauli ya ‘kutomwacha yeyote nyuma’ siyo msemo tu bali ni wito wa kuwawezesha watu, kuwapa sauti na kuhakikisha ushirikishwaji na usawa.Ni wito wa kuondoa pengo katika kipato na fursa. Na katika usiku huu wa kuamkia Siku ya kimataifa ya Wanawake ni wito pia wa kuondoa pengo na jinsia.” Amesisitiza.

Akimnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Naibu Katibu amesisitiza, “sikubaliani na dunia ambayo inawaambia wajukuu zangu kuwa usawa wa kiuchumi unaweza kusubiri kwa ajili ya wajukuu wa wajuu zao. Tunajikongoja kufikia ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma”

Aidha amesema, “tunasema vijana ni mstakabali wa siku za usoni lakini ukosefu wa ajira uko katika kiwango cha juu”

Amemalizia kwa kueleza juu ya matumaini yake kuwa kwa pamoja dunia inaweza kufikia hatua ambayo hakuna aliyeachwa nyuma, “Asanteni kwa uongozi wenu na tuendelee kuwa na matumaini kwa ajili ya mamilioni ya watu ambao kila siku wanaishi maisha ya njaa, hofu, mateso, vurugu, kunyanyaswa na kuuawa.”