Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zaidi zahitajika kulinda wasichana barubaru dhidi ya VVU- UNAIDS

Gloria ambaye anaishi na virusi vya ukimwi katika vitongoji vya Khayelitsha mji wa Cape Town, Afrika Kusini ambako kampeni ya kuchagiza uelewa wa ukimwi ilifanyika mano Agosti 2007.
World Bank/Trevor Samson
Gloria ambaye anaishi na virusi vya ukimwi katika vitongoji vya Khayelitsha mji wa Cape Town, Afrika Kusini ambako kampeni ya kuchagiza uelewa wa ukimwi ilifanyika mano Agosti 2007.

Hatua zaidi zahitajika kulinda wasichana barubaru dhidi ya VVU- UNAIDS

Afya

Kila siku wasichana barubaru 460 duniani kote wanaambukizwa Virusi Vya Ukimwi, VVU ilhali wengine 350 hufariki dunia kila wiki kutokana na Ukimwi na magonjwa yahusianayo na ugonjwa huo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Ukimwi, UNAIDS hii leo,

Ikiwa ni taarifa iliyotolewa leo huo Geneva, Uswisi kuelekea siku ya wanawake duniani kesho Machi 8, UNAIDS inasema ni lazima serikali ziimarishe juhudi za kulinda vijana wa kike na wasichana barubaru dhidi ya maambukizi ya VVU.

UNAIDS inasema magonjwa yahusianayo na Ukimwi yamesalia sababu kuu ya vifo miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 duniani kote, ambapo mwaka 2017 pekee asilimia 66 ya maambukizi mapya ya VVU kati ya watu wenye umri wa miaka 10 hadi 19 walitoka eneo la mashariki na kusini mwa Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibe amesema sababu ya mwenendeo huo ni kuwepo kwa mzunguko hatari wa ukosefu wa usawa wa jinsia, ukatili wa kijinsia na maambukizi ya VVU katika sehemu nyingi duniani.

Amesema ni lazima ukandamizaji na ukosefu wa mizania ya mamlaka vibadilishwe sambamba na mila potofu za mfumo dume ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanakuwa na usemi kamilifu juu ya haki zao za afya ya uzazi.

Bwana Sidibe amesema harakati za kutokomeza Ukimwi miongoni mwa vijana wa kike na wasichana barubaru zinagonga mwamba pindi haki zao za afya ya uzazi haziungwi mkono.

Amesema sheria ya kimataifa inawapatia wato wote wakiwemo kundi hilo haki ya kupata huduma za kujikinga kwenye ngono na pia huduma za afya ya uzazi.

Amepigia chepuo hatua zilizochukuliwa na nchi kama vile Uganda za kujumuisha elimu ya masuala ya afya ya uzazi shuleni akisema imezaa  matunda katika kulinda wasichana dhidi ya maambukizi ya VVU.